Na Mashaka Mgeta, MOROGORO
WATUMISHI wa umma wametakiwa kuboresha nyanja za utoaji huduma kwa wananchi, ili kuendana na ubora na thamani ya miradi ya maendeleo inayogharamiwa na Serikali katika kuchagiza ustawi wao.
Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Beatrice Kimoleta, amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya uandaaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja,) na kuwahusisha Makatibu Tawala Wasaidizi (Utawala na Rasilimali Watu) na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kutoka ofisi za wakuu wa mikoa nchini.
Mafunzo hayo yanayotolewa kwa ushirikiano wa TAMISEMI na Ofisi ya Rais (Utumishi), yanafanyika kwenye Chuo Kilimo cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro.
Kimoleta amesema, Serikali imefanikiwa kujenga na kuboresha miundombinu kupitia miradi inayogharimu fedha nyingi, hivyo utoaji huduma kwa wananchi unapaswa kuakisi ukubwa wa hatua za maendeleo zilizofikiwa na zinazoendelea kutekelezwa.
Kwa mujibu wa Kimoleta, wakati kuna dalili za wananchi wengi kuridhishwa na miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya kisekta, mwelekeo uliopo kwao (wananchi) ni dhidi ya watumishi wa umma, kwa namna wanayotekeleza majukumu katika kuwahudumia.
‘’Hivi sasa kuna mabadiliko makubwa, wananchi wanatufuatilia (watumishi wa umma) jinsi tunavyotoa huduma zetu, na wasiporidhika, inakuwa mwanzo wa kuibua malalamiko kwa njia wanazoziona zinawafaa, ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii,’’ amesema na kusisitiza umuhimu wa utoaji huduma bora kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Nteghenjwa Hosseah, amewahimiza Maafisa Mawasiliano Serikalini hususani katika Sekretarieti za Mikoa, kuimarisha ushirikiano na Maafisa Habari wa Halmashauri na vyombo vya habari, ili kufanikisha azma ya Serikali kwa wananchi kupata habari zilizo sahihi na za kweli.
Hosseah, ameyasema hayo alipokuatana na Maafisa Mawasiliano Serikalini wakati wa mafunzo ya uandaaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja yanayofanyika kunzia januari 29,2025 na kufikia kilele chake kesho Februari 1, 2025.
Amesema Serikali imeboresha mazingira ya maafisa mawasiliano serikalini kwa kiasi kikubwa, hivyo wakati maboresho zaidi yakiendelea, wataalamu hao wa mawasilianoo wanapaswa kuhakikisha azma ya umma kupata taarifa sahihi na kweli inafikiwa.
Hosseah amesema miongoni mwa maeneo ambayo serikali imewekeza na kutumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu na vifaa ni pamoja sekta za elimu, afya, miundombinu na utawala bora.
Amewahimiza Maafisa Mawasiliano Serikalini na Maafisa Habari wa Halmashauri, kujiwajibisha katika utendaji wenye kukidhi weledi wa taaluma yao, kuandika na kutangaza habari zilizochakatwa na kutolewa tafsiri zinazotokana na matumizi ya takwimu.
Afisa Mawasiliano wa Serikali wa mkoa wa Katavi, Ambwene Mwaifuge, amesema mafunzo hayo, na ushirikishwaji unaofanyika kwa nyakati na matukio tofauti serikalini, umekuwa sehemu ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao, ikiwemo kufikisha taarifa sahihi na habari za kweli kwa umma.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.