Na Mashaka Mgeta, KILINDI
WAKAZI wa kijiji cha Kwekinkwembe katika wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, wamesema ukosefu wa elimu na uelewa duni wa kusoma ramani, unachochea migogoro ya ardhi hasa inayohusu mipaka ya vijiji.
Wamesema hayo katika mkutano ulioitishwa kijijini hapo jana Julai 2, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian.
Lengo la mkutano huo uliotanguliwa na mwingine uliofanyika kwenye kijiji cha Lengusero, ni kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka wa vijiji hivyo, uliosababisha kutotekelezwa kwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kijijini Kwekinkwembe.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwekinkwembe, Shaban Omar amesema, kutofahamu tafsiri ya mipaka, kumechangia pia uongozi na wakazi wa kijiji chake, kushindwa kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa upimaji, na hivyo kusababisha Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi usitekelezwe kijijini humo.
”Hatujawahi kupinga utekelezaji wa Mpango, kilichotokea ni kutaka kujua uhakika wa ramani iliyotumika na hapo ndipo changamoto ilipoanzia,” akasema.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho, Saidina Ali akasema ukosefu wa elimu ya kutafsiri ramani inasawaingiza viongozi wa vijiji katika hatari ya kufanya maamuzi yakiwemo ya uuzaji ama uidhinishaji mauzo ya ardhi kinyume cha taratibu.
Vijana kadhaa wa kijiji hicho, wamepongeza hatua ya Mhe Balozi Dkt Batilda kufanikisha upatinaji suluhu wa mgogoro uliokuwepo, kwamba utawasaidia kushiriki shughuli za uzalishaji kadri ya matumizi ya ardhi yatakavyopangwa.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Lengusero, Julius Lorkime, akasema mauzo ya ardhi ya kijiji hicho yaliyofanywa na watu ama kuidhinishwa na viongozi wa Kwekinkwembe
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, vitendo vinavyokwamisha utekelezaji wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ni kinyume cha Sheria na ukwamishaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan.
Amesema uongozi wa mkoa unafuatilia kwa karibu kuwabaini wachochezi na wanaosababisha migogoro ya ardhi mkoani humo, ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Pia Mhe Balozi Dkt Batilda akawahimiza wakazi hao kusimamia amani na utulivu kama sehemu ya nyenzo muhimu kufanikisha maendeleo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe Hashim Mgandilwa, akasema mgogoro uliokuwepo haukuwa na mashiko kwa vile ramani ya mwaka 1993 wanayoikubali wakazi wa Kwekinkwembe, inafanana na ile ya mwaka 2007 iliyowasilishwa na wataalamu wa ardhi na upimaji.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.