Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
KABLA ya Februari 27, 2027, jina msichana Ester Barua, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Magila wilayani Muheza, halikujulikana kwa umma mpana.
Hatua ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, aliposimama na kumpisha kwenye kiti chake, japo kwa dakika chache, kikamfanya mwanafunzi huyo mwenye umahiri wa kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha kujulikana na kuwavutia wengi.
Ni msichana aliyekuwa miongoni mwa maelfu ya wakazi wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga, waliofika kwenye uwanja wa Jitegemee, kumsikiliza Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Pamoja na mambo mengine, Mhe Rais Dkt Samia alifika wilayani humo kuzindua usambazaji mitungi ya gesi ya kupikia na majiko banifu kwa bei ya ruzuku iliyofanyika Muheza mkoani Tanga.
Hafla hiyo ikawashuhudia wasanii wa burudani wakitumbuiza, na baadaye wakaingia watoto walioigiza sauti za marais wastaafu.
Hapo ndipo Ester alipoonesha kipaji na uwezo thabiti kuelezea ukweli wa miradi mikubwa ya kimkakati, inayotekelezwa na Serikali ya Mh Rais Dkt Samia kwa Kiingereza.
Akitumia ufasaha wa lugha hiyo, Ester akaainisha mradi mmoja hadi mwingine, kisha kuweka wazi kiu na ndoto yake ya kuwa Rais kwa miaka ijayo.
Kuanzia hapo, Ester akawa kivutio kwa washiriki wa mkutano huo, wakiwemo viongozi na waandishi wa Habari.
Ester alizaliwa Mei 31, 2009 kwenye kijiji cha Kiumba Magila wilayani Muheza. Ni mtoto wa tatu kati ya watoto saba wa familia yake.
Anapozungumzia mambo anayoyapenda, Ester anataja kusoma na kusikiliza muziki wenye ujumbe wa kimaadili, kuwa ndivyo anavyopendelea zaidi.
Anavyoifahamu miradi
Msichana huyo anasema, uongozi wa Mhe Rais Dkt Samia unamvutia sana hasa kwa namna anavyobuni na kutekeleza miradi na huduma zenye tija kwa wananchi walio wengi.
Ester anasema, anazipata taarifa zinazohusiana na miradi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Anasema, kwa namna ilivyo muhimu kuijua miradi hiyo na manufaa yake kwa jamii, amekuwa akimuomba Mwenyezi Mungu amfungulie hekima, busara na maarifa kuitangaza kwa wananchi walio wengi.
“Nina ndoto za kuwa Daktari wa binadamu, lakini pia kuwa kiongozi wa ngazi ya juu kama Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’’anasema.
Ester anasema, Mhe Rais Dkt Samia ni mwanamke jasiri anayeipambania nchi yake (Tanzania) kwa dhati na kuongeza…
‘’Mimi ninajivunia sana kuwa kwenye nchi hii ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,’’ anasema.
Anapoulizwa kuhusu ujumbe wake kwa Watanzania, anasema ‘’kwanza kwa wanafunzi wenzangu, wajiamini na wasiogope kutoa kitu ambacho wanacho moyoni, eti kwa sababu watachekwa,’’ anasema.
Anaongeza, ‘’kuchekwa kupo tu, hata mimi mwenyewe hapa nimeshachekwa sana. Kwa wazazi, ninawaomba wawasaidie watoto wao kutimiza ndoto zao za baadaye.’’
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.