MUHEZA WANUFAIKA NA MAJI YA BOMBA LA EACOP
Na Mashaka Mgeta, MUHEZA
DHANA ya ‘mgeni njoo mwenyeji apone’, imeoneka katika wilaya ya Muheza, ambapo mradi wa maji wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda kwenda Chongoleani mkoani Tanga (EACOP), sasa utawanufaisha wakazi wa kata nne kati ya 37 zilizopo wilayani humo.
Taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga UWASA) iliyosomwa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava, imeeleza kuwa mradi huo, awali, utekelezaji wa mradi ulihusisha ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha inchi nne.
Lakini, kutokana na kubainika umuhimu wa wakazi wa maeneo bomba hilo la maji linapopita, kuwa sehemu ya wanufaika wake, maboresho yalifanyika kwa kuongeza ukubwa wa kipenyo kufikia inchi tisa na hivyo kuibuliwa kwa mradi huo uliopo eneo la Michungwani, kata ya Genge.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2024, Mnzava, amesema hatua ya kuwafikishia wananchi huduma za jamii ikiwemo maji, inaakisi dhamira, utashi na utayari wa Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwaondolea wananchi kero zinazowafanya wakose huduma wanazozistahili.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah amesema, pamoja na serikali kuwaunganishia wananchi maji kutoka kwenye bomba la maji la EACOP, Muheza itanufaika kwa kupata sehemu ya mradi wa maji kwenye miji 28 utakaogharimu takribani Shilingi bilioni 40 kwa wilaya hiyo pekee.
Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma, anathibitisha kwamba mradi huo wa miji 28 utaondoa kero ya maji wilayani humo.
Taarifa ya Meneja wa Tanga UWASA, kanda ya Muheza, Mhandisi Ramadhani Nyambuka, imeeleza kuwa mradi huo uliogharimu Shilingi 532,550,000 na kutekelezwa na mkandarasi, Sajo Civil Engineering and Building Construction Company, unalenga kuboresha upatikanaji wa majisafi katika kata za Lusanga, Genge, Majengo na Tanganyika zenye jumla ya wakazi 21,721.
Amesema, utekelezaji wa mradi huo ulianza Januari, 2023 na kukamilika kwa asilimia 100, Septemba, 2023 ukihusisha uchimbaji wa mtaro mita 6000, ununuzi na ulazaji wa bomba lenye kipenyo cha milimita 200 kwa urefu wa mita 6000, ununuzi na ufungaji wa viungio vya mabomba, ujenzi wa chemba 15 na ujenzi wa alama za bomba 76.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.