KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Ndugu Mnzava ameisifu Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) mkoa wa Tanga, kwa kutimiza takwa la kisheria kutangaza zabuni za miradi yake kwenye mfumo wa manunuzi ya umma.
Ndugu Mnzava amesema, hatua hiyo inatoa ishara ya umuhimu wa mifumo ya manunuzi ya umma kujulikana kwa watendaji wa serikali katika ngazi zote, na kwa wajumbe wa Kamati za Usalama (KU) ili kuwa na uelewa wa pamoja katika usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya umma.
Ameyasema hayo baada ya kukagua mradi wa maji Magila Gereza, wakati Mwenge wa Uhuru 2024 wenye ujumbe unaosema, ‘Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu’ ukiwa katika siku yake ya kwanza mkoani Tanga.
Kuhusu mradi wa maji Magila Gereza, Ndugu Mnzava amesema pamoja na ubora wake, inapaswa kuongezewa nyenzo za ulinzi na usalama kwenye chanzo cha maji na tenki lililopo.
Amesema licha ya RUWASA kuendelea kutoa elimu kuhusu ulinzi shirikishi kwenye chanzo cha maji na tenki la mradi huo, jeshi la polisi kupitia kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Korogwe, linapaswa kuwajengea uwezo wananchi kuhusu mbinu za ulinzi kwenye chanzo cha maji na tenki lililopo.
Pia, Ndugu Mnzava amewahimiza wananchi wa Korogwe kuyalinda na kuyahifadhi mazingira ya safu ya milima ya Usambara yenye vyanzo vingi vya maji, kwa vile maji hayo ni safi, salama na yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Korogwe, Mhandisi William Tupa, amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi 775,743,809 zilizotolewa kupitia Mfuko wa Maji (NWF), unawahudumia watu 4,543 katika vijiji vya Magila Gereza, Nkalekwa na Mgobe.
Mhandisi Tupa amesema kazi zilizopangwa na kutekelezwa kwenye mradi huo ni ujenzi wa chanzo cha maji uliofikia asilimia 95, tenki la ujazo wa lita 300,000 (asilimia 95), mtaro na kufunga mabomba mita 26,314 (asilimia 80), vilula 28 (asilimia 90) na alama za njia za bomba 264 (asilimia 20).
Habari hii imeandikwa na Mashaka Mgeta wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.