Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
HATARI ya kushindwa kutekeleza miradi yenye tija kwa jamii, kunakofanywa na Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs), kutapata suluhu kupitia mpango wa kupanua wigo wa wafadhili na kuanzisha miradi yenye ubunifu.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, ameyasema hayo leo Agosti 6, 2025, alipokuwa anafungua Mkutano wa Mwaka wa Mashirika hayo mkoani humo.
Amesema, kutokana na mabadiliko ya utekelezaji wa sera za nje kwa baadhi ya nchi wafadhili, sehemu ya NGOs imejikuta ikikosa ruzuku na hivyo kuwa katika hatari ya kushindwa kutekeleza majukumu yao yanayotambuliwa kikatiba.
Kwa hali hiyo, Mhe Balozi Dkt Batilda, ameziasa NGOs kutotegemea wafadhili kutoka upande mmoja wa dunia, bali kutazama na mataifa mengine yenye uwezo na nia kusaidia miradi ya maendeleo na ustawi wa watu kwa nchi zinazoendelea.
Pia, Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, ingawa NGOs hazipaswi, kwa mujibu sheria, kufanya biashara zenye kuzalisha faida, zinaweza kuwa na miradi bunifu itakayowawezesha kumudu kujiendesha kupitia huduma wanazozitoa.
Mhe Balozi Dkt Batilda ametoa rai kwa NGOs kuwekeza katika matumizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuwianisha shughuli zao na mipango ya Serikali katika kuwatumikia wananchi.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tanga, Gloria Maleo, amesema kati ya mashirika 315 yaliyopo mkoani humo, ni 50 pekee (sawa na asilimia 15.9) yanayotekeleza miradi ya maendeleo.
Maleo amesema sekta zinazohudumiwa kwa kiasi kikubwa na NGOs hizo ni afya, elimu, ulinzi wa kijamii, uwezeshaji wananchi kiuchumi, kiliko, utawala bora, mazingira, maji, jinsia na haki za binadamu.
Hata hivyo, Maleo amesema sehemu kubwa ya NGOs hizo zinashindwa kufanya kazi kwa kufuata mifumo ya kieletroniki, hivyo kutoandaa taarifa za utekelezaji na marejesho ya fedha wanazotumia.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.