Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
ASASI zisizokuwa za kiserikali mkoani Tanga, zimeaswa kudhibi vitendo vyenye kuashiria mmomonyoko wa maadili kama matumizi ya dawa za kulevya, unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
Kabla ya kutekeleza jukumu hilo, asasi hizo zimeshauriwa kufanya utafiti wa kina kwenye jamii, ili kubaini, kupendekeza na kuchua hatua dhidi ya vitendo hivyo, ambavyo kwa mujibu wa taarifa za vyanzo mbalimbali, kasi yake inaongezeka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali, Mwantumu Mahiza, ametoa rai hiyo alipozungumza kwenye Mkutano wa Mwaka wa Mashirika hayo mkoani Tanga, leo Agosti 6, 2025.
Amesema, Tanga ni miongoni mwa mikoa minne nchini inayotajwa katika kushamiri kwa vitendo hivyo, hivyo ipo haja ya kuunganisha nguvu kwa sekta za umma na binafsi, kudhibiti hali hiyo.
Kwa mujibu wa Mahiza, vitendo hivyo vinawahusisha zaidi vijana walio nguvu kazi kwenye kaya, jamii na taifa na kuongeza, “fanyeni utafiti kubaini kwa sababu gani idadi ya wahusika hawa inaongezeka.”
Amesema, sababu iliyozoeleka kuhusu hali duni ya kiuchumi, haina mashiko kwa vile Tanga imejaliwa kwa rasilimali kama vile ardhi yenye rutuba, mvua za mara mbili kwa mwaka, bahari, mifugo, miongoni mwa nyingine nyingi.
Pia, ameasa jamii kushiriki katika udhibiti wa vitendo hivyo, ikiwemo kuacha kupindisha msingi wa utamaduni uliotumika kama, kama matumizi ya ngoma za asili zilizokuwa zinachezwa nyakati za jando na unyago.
Amesema ngoma hizo zilizojulikana kama “ngoma za ndani”, hivi sasa zimebadilishwa kwa mapigo na maudhui, mfano wake ukiwa ni vigoma vua uruguai na vijamvi.
“Wakati tukiidhibiti hali hii, tuendelee kuwaelimisha vijana washiri kutenda mambo yaliyo mema, na kuwasaidia ili wafikie ndoto njema za kuwa na maisha bora ya sasa na baadaye,” amesema.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.