Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
DHAMIRA ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuirejesha Tanga kuwa ’Mkoa wa Viwanda’ hailengi kuinua uchumi na kuboresha maisha ya watu pekee, bali pia kurejesha bidhaa zilizoanza kusahaulika kwenye masoko.
Miongoni mwa bidhaa hizo ni sabuni aina ya Foma, iliyowahi kutumika kwa miaka kadhaa iliyopita, ikisifika kwa ubora na povu lake katika kufulia nguo na kusafishia vyombo.
Jana Agosti 4, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amekitembelea kiwanda cha kampuni ya Africa Harmony Industry Limited, pamoja na mambo mengine, kubaini changamoto zilizokwamisha utekelezaji wa ahadi ya kuanza uzalishaji Aprili mwaka huu.
Akiwa na wajumbe wa Kamati ya Usalama (KU) ya mkoa huo, Mhe Balozi Dkt Batilda, amekutana na wawakilishi wa menejimenti ya kiwanda hicho, na kupitia kwa Afisa Rasilimali wake, Ahmed Mustapha, imethibitika kuwa uzalishaji huo utaanza Oktoba mwaka huu.
Mustapha ambaye pia alimtembeza Mhe Balozi Dkt Batilda na ujumbe wake kukagua maandalizi ya kuboresha kiwanda hicho kabla ya kuanza kazi, amesema zipo changamoto mbalimbali zilizosababisha kukwama kwa uzalishaji Aprili, lakini kwa maandalizi yanayoendelea, uwezekano wa kuanza Oktoba upo kwa asilimia 100.
Ujumbe wa Mhe Balozi Dkt Batilda, umeshuhudia sehemu ya vijana wanaotajwa kufikia 100, wakishiriki kwenye hatua tofauti za maandalizi na uboreshaji wa miundombinu ya kiwanda hicho.
Mhe Balozi Dkt Batilda, ameiagiza menejimenti ya kiwanda hicho, kuhakikisha inatimiza masharti ya kutoa kipaumbele cha ajira za kudumu na mikataba kwa wakazi wa Tanga hususani vijana na wanawake wenye vigezo.
Kabla ya kukitembelea kiwanda hicho, Mhe Balozi Dkt Batilda alitembelea kKwanda cha Saruji cha Tanga na kuzungumzia masuala mbalimbali ya ukuzaji uzalishaji, biashara na utanuzi wa shughuli za kiwanda hicho.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.