Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
MATANGAZO ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) asubuhi ya leo Machi 27, 2025, yamemtaja Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa kielelezo cha viongozi bora wanawake wanaoleta mabadiliko chanya barani Afrika hususani kwa vijana.
Kupitia sehemu ya Gumzo ya kipindi cha Amka na BBC, Mhe Rais Dk Samia ametajwa wakati mada inayohusu ‘Kuchaguliwa kwa Netumbo Nandi-Ndaitwah kuiongoza Namibia na Uongozi wa Wanawake barani Afrika’.
Desemba 3, 2024, Mhe Nandi-Ndaitwah alitangazwa na Mwenyeiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Namibia (ECN), Elsie Nghikembua kushinda urais, hivyo kuunda Baraza la Mawaziri na kumteua Lucia Witbooi, kuwa Makamu wa Rais mwanamke wa kwanza tangu taifa hilo kupata Uhuru wake Machi 21,1990.
Kipindi hicho kilichoongozwa na Mtangazaji raia wa Kenya, Sarafina Robi na kuhusisha wachangia mada, mwanaharakati Hamisa Zaja wa Kenya na Mwanahabari Nixon Katembo kutokea Afrika Kusini.
Zaja amesema harakati za ‘kupigania’ nafasi ya mwanamke katika uongozi barani Afrika imechukua muda mrefu, hivyo kusikia Rais, Makamu wa Rais na Mawaziri kadhaa ni wanawake, ni jambo la faraja.
Kuhusu matarajio ya raia wa Namibia kwa Mhe Rais Nandi-Ndaitwah, Zaja amesema anapaswa kutoa matokeo chanya kwao (wananchi), akitoa mfano wa mafanikio ya Mhe Rais Dkt Samia katika nyanja mbalimbali za kijamii.
Zaja ametaja sehemu ya mafanikio ya Mhe Rais Dkt Samia aliyeingia madarakani Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, ni uwekezaji katika ujasiriamali hasa kwa vijana.
“Tufanye tu mfano mfupi, hata Makamu wa Rais ambaye kwa sasa ni Rais wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu, kitu cha kwanza ambacho amekifanya, amewekeza ujasiriamali kwa vijana wadogo, katika kuweka (kutekeleza) ahadi zake…’’
‘’Tumuangalie tena kwa sababu ni mama, anajua zile shida, unajua mama ni mtu ambaye anazijua zile shida za kilimo, umiliki wa ardhi hasa kwa akina mama, mila na desturi hazijampatia umiliki wa ardhi,’’ amesema akianisha umahiri wa uongozi wa Mhe Rais Dkt Samia.
Kwa hali hiyo, Zaja amesema, Mhe Rais Nandi-Ndaitwah wa Namibia, anapaswa kuhakikisha hatua kama umiliki mkubwa wa ardhi kwa wanawake zinafikiwa.
Ametaja hatua nyingine kuwa ni kwa viongozi wanawake kuleta mageuzi ya kiutendaji zaidi ya asilimia 50 ya viongozi wanaume, ili kuimarisha imani ya umma kwao.
Naye Katembo amesema kuchaguliwa kwa Mhe Rais Nandi-Ndaitwah kumechangiwa na historia ya umahiri wake katika nafasi mbalimbali za utumishi wa umma alizozitumikia.
Amesema, ili kuaminika na kuchaguliwa kushika nafasi kubwa ya uongozi ikiwemo Urais, kukubalika, ushupavu na umahiri ni mambo ya msingi kutazamwa.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.