Serikali imeendelea kuboresha sekta ya Afya kwa kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa, na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za Afya. Aidha, bajeti ya Mkoa kwa ajili ya kugharimia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi imeongezwa kutoka shilingi bilioni 1.8 mwaka 2015/2016 na kufikia shilingi bilioni 8.7 mwaka 2019/2020.
Hili ni ongezeko la shilingi bilioni 6.9 sawa na asilimia 79.3. Kwa upatikanaji wa dawa muhimu (Essential medicines) kwa mwaka 2015/2016 ulikuwa asilimia 92 na kwa mwaka 2019/2020 ni asilimia 95 naupatikanaji wa dawa viashiria (Tracer medicines) kwa mwaka 2015/2016 ulikuwa asilimia 94.4 ikilinganishwa na asilimia 98 kwa mwaka 2019/2020 katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Mkoa.
Sambamba na upatikanaji wa dawa muhimu, Hadi kufikia mwaka 2015 Mkoa wa Tanga ulikuwa na vituo vya kutolea huduma 369; Hospitali 10, vituo vya Afya 38 na Zahanati 321. Kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 Mkoa wa Tanga una vituo vya kutolea huduma 400; ambapo Hospitali zipo 11, vituo vya Afya 41, Zahanati 348. Aidha, Mkoa wa Tanga tumepokea Sh. Billion 14.1 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali tatu za Wilaya ya Tanga Jiji, Muheza na Korogwe Vijijini na vituo vya Afya 22.