DK SAMIA AWAHIMIZA WAUGUZI KUFANYA KAZI KWA BIDII
Na Mashaka Mgeta, OMM – TANGA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dk Samia Suluhu Hassan, amewaagiza wauguzi kote nchini, kufanya kazi kwa bidii, na kwamba anazitambua changamoto zinazowakabili na ambazo anazichukua ili kuzipatia suluhu ya kudumu.
Mhe Rais Dk Samia ameyasema hayo kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe Mohamed Mchengerwa, alipokuwa akizungumza kwenye Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 51 wa Chama cha Wauguzi na Wakunga (TNNA) unaofanyika mjini hapa.
‘’Mhe Rais Dk Samia ameniagiza niwaeleze kwamba anatambua kuwa taaluma yenu ina umuhimu mkubwa sana kwa maisha ya watu nchini na duniani, hivyo fanyeni kazi kwa bidii na changamoto zenu anazitambua na anazifanyia kazi,’’ amesema huku akishangiliwa na maelfu ya wauguzi wanaohudhuria mkutano huo.
Miongoni mwa changamoto zinazoainishwa na wauguzi zinahusiana na kutopandishwa madaraja, kutolipwa stahili zao kwa wakati wanaposhiriki mkutano huo, kupokwa uhuru wa kitaaluma, ‘kuchakachua’ vigezo kwa wanafunzi wanaojiunga kusomea taaluma hiyo, miongoni mwa changamoto kadhaa.
Hata hivyo, Mhe Mchengerwa amemuagiza Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dk Rashid Mfaume, kukaa na viongozi wa TANNA na wadau wengine, kuhakikisha changamoto hizo hususani zinazohusiana na kutopandishwa madaraja, zinapata suluhu ndani ya wiki mbili kuanzia Mei 9, 2024.
Mhe Mchengerwa amesema, Mhe Rais Dk Samia amefanikiwa kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha zilizofanikisha ujenzi wa miundombinu, vifaa tiba, makazi ya wataalamu wa afya, hivyo hakuna sababu ya kuweka mazingira yanayowakatisha tamaa wauguzi na wataalamu wa afya nchini.
Amesema mafanikio mengine ya Mhe Rais Dk Samia ni kutengeneza ajira mpya 25,206 katika sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu aliyopo madarakani, ikihusisha ujenzi wa miundombinu ya hospitali za wilaya, vituo za afya, zahanati na ununuzi wa vifaa tiba ikiwemo mitambo 21,000 ya hewa tiba.
Hivyo, amewaasa wataalamu wa afya wakiwemo wauguzi kutimiza wajibu wao ipasavyo, kwa vile uwepo wa miundombinu pasipo upatikanaji wa huduma bora za afya haitakuwa na maana kwa wananchi.
Mhe Mchengerwa amehimiza utendaji kazi unaokidhi matakwa ya haki, usawa na upendo kwa wagonjwa, na ili kuchagiza uendelevu wa hali hiyo, amewaagiza washiriki wa kongamano na mkutano huo kula kiapo cha utoaji huduma bora, hatua itayofanyika kwenye kilele cha kongamano na mkutano huo Jumapili na kuhudhuriwa na Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu.
Mwenyekiti wa TANNA, Alexanda Baluya ametoa rai kwa wauguzi kujikita katika utendaji wa majukumu yao na kujitenga na masuala yasiyohusika na taaluma ya uuguzi; na ametoa rai kwa mamlaka husika kutoa ulinzi kwa wauguzi wanapotekeleza majukumu yao, ikiwa ni sehemu ya kuwahakikishia usalama zaidi wanapokuwa kazini.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi katika Wizara ya Afya, Ziada Sellah amewashauri wauguzi kujiendeleza kielimu na kitaaluma, ili kuboresha zaidi utoaji huduma za uuguzi zinazochukua takribani asilimia 80 ya huduma za tiba kwa wagonjwa.
Naye Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dk Rashid Mfaume, amehimiza umuhimu wa Serikali kuwawezesha wauguzi kupata posho zinazotokana na hatari zinazowakabili wanapokuwa kazini na ongezeko la mishahara yao.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amesema mkoa huo umepokea kiasi kikubwa cha fedha kwa miradi ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya afya, na kwamba uongozi wake unaendelea kusimamia na kufuatilia ili iwe na tija kwa umma mpana.
Hata hivyo, Mhe Balozi Dk Batilda amesema mkoa huo unakabiliwa na upungufu wa wataalamu wakiwemo wahandisi, wakaguzi wa ndani na wataalamu wa afya, ingawa Serikali ya Mhe Rais Dk Samia inaendelea kutoa ajira mpya zinazounufaisha mkoa huo katika kukabiliana na changamoto hizo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.