Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
NI dhahiri mwaka 2024 unamalizika kwa orodha ya rekodi katika nyanja tofauti za kijamii, ambapo, mkoani Tanga, Tamasha la Urithi wa Utamaduni Wetu likiwa la kwanza kufanyika, linaweka historia itakayodumu.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, anaratibu tamasha hilo linaloshirikisha wadau wengine zikiwemo halmashauri za wilaya, miji na jiji, wajasiriamali, wawekezaji katika tasnia za utalii, biashara na uvumbuzi, wasanii, wabunifu, familia na jumuiya zenye shauku ya kusherehekea pamoja.
Mhe Balozi Dk Batilda, anakutana na waandishi wa habari ofisini kwake jana Desemba 24, 2024, na kutangaza kuwa tamasha hilo litafanyika kwa matukio ya ‘bandika – bandua’, kuanzia Desemba 27, 2024 hadi Januari Mosi, mwaka ujao.
Akiwa na timu ya uratibu wa tamasha hilo kutoka sekta za umma na binafsi, Mhe Balozi Dk Batilda, anasema lengo kuu ni kutunza na kutengeneza jamii inayochangamkia fursa za urithi wa utamaduni katika mandhari nzuri ya mkoa huo na ukanda wa pwani kwa ujumla.
WASHIRIKI KUTOKA MIKOANI, NCHI JIRANI KUHUDHURIA
Mhe Balozi Dk Batilda anasema, tamasha hilo linatazamiwa kuwaleta pamoja watu kutoka mikoa na nchi mbalimbali, wakiwakilisha nyanja zote za maisha, kusherehekea, kukuza urithi, kuheshimu mila, tamaduni , desturi na kukumbatia ubunifu na uzalendo uliopo nchini.
KITOVU CHA UTAMADUNI NA BIASHARA
Mhe Balozi Dk Batilda anaweka bayana kwamba, Tanga ni kitivo cha utamaduni na biashara, hivyo kuufanya mkoa huo kuwa mahali pazuri kwa tamasha hilo na mandhari yake ya kuvutia usanifu wa kihistoria na uwekezaji.
UHONDO UTAKAOHANIKIZWA
Mambo mengi mazuri yenye kuvutia, kuburudisha, kufundisha na kurithisha utamaduni wa Tanga yatafanyika wakati wote wa tamasha hilo, kama anavyobainisha Mhe Balozi Dk Batilda.
Mhe Balozi Dk Batilda anayataja mambo hayo kuwa ni pamoja na ngoma za asili, maonesho ya vyakula vya asili ya Tanga, ziara za kihistoria, sanaa, ustaarabu wa pwani, uchumi wa buluu na kazi za ubunifu wa bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia katani na ukindu.
Kwa mujibu wa Mhe Balozi Dk Batilda, tamasha hilo litahusisha pia burudani asilia na usiku wa khanga za kale, usiku wa alwatan, usiku wa mvuvi. Vyote hivyo vitapambwa na mavazi ya asili kama khanga za kale, baibui la ukaya, misuli na barakhashia.
KAMA HUJAWAHI KUNYWA CHAI YA KUKAANGA, HII INAKUHUSU
Mhe Balozi Dk Batilda anasema aina ya chai zisizopatikana kwenye maeneo mengine ya nchi, ni miongoni mwa bidhaa zinazolifanya tamasha hilo kuwa la kipekee, na kuwaalika watu wengi zaidi kushiriki ili kuzishuhudia na kunywa chai hizo ikiwa ni pamoja na zinazotengenezwa na nazi, pilipili na chai ya kukaangwa.
‘’Tunachukua fursa hii kuwakaribisha wote kushiriki nasi, kwani kuijua Tanga ni kuonja chakula chake, kusikia muziki na sauti zake na kutembelea historia yake, mahali ambapo zamani na sasa vinacheza pamoja,’’ amesema Mhe Balozi.
WAWEKEZAJI WASIKAE KANDO…WAJE TANGA
Mhe Balozi Dk Batilda anasema kwa upande wa wawekezaji, Tanga ni eneo mahususi la ki-mkakati, ikiwa na fursa nyingi, ukaribu wake na njia kuu za biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, bandari yenye kina kirefu na miundombinu iliyo bora, ni miongoni mwa mazingira yanayochochea uwekezaji, biashara na utamaduni.
‘’Tamasha hili linatumika kama daraja la kufungua uwezo wa kiuchumi wa Tanga, huku likisherehekea maisha yake ya sasa na ya zamani,’’ amesema Mhe Balozi Dk Batilda.
NUKUU YA SHABAN ROBERT
Mhe Balozi Dk Batilda, anamnukuu Mwandishi nguli wa vitabu na riwaya, marehemu Shaban Robert aliposema, urithi wa Tanga sio tu katika magofu yake ya zamani, au mitaa ya namba ya ukoloni, lakini katika hadithi zinazonong’onezeka kwa vizazi.
Mhe Balozi Dk Batilda anasema, dhana hiyo imechochea kuwepo kwa tamasha hilo, ili kurithisha utamaduni wa Tanga na kwa hali hiyo, Januari Mosi, 2025 kutakuwa na Kongamano la Kumbukumbu ya Shaban Robert.
RUZUKU YA WAZO BUNIFU
Mhe Balozi Dk Batilda, anasema pamoja na mema mengi ya kitamaduni yatakayofanyika kwenye tamasha hilo, kutatolewa tuzo ya ruzuku ya wazo bunifu la biashara kwa vijana, wanawake na wazee.
Amesema mawazo bunifu tofauti yatashindanishwa, yakiwa na viwango tofauti vya mtaji na kwamba ruzuku itakayotolewa kwenye mawazo husika, itaanzia Shilingi 100,000 hadi milioni 1.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.