Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
KATIBU Tawala Mkoa (RAS) wa Tanga, Pili Mnyema, amewataka watumishi wa umma mkoani humo, kutii na kutekeleza maagizo ya mamlaka zao, ili kuendeleza na kuimarisha mifumo ya utendaji inayochochea ufanisi, maendeleo na ustawi wa watu.
Mnyema ameyasema hayo jana Desemba 18, 2024 alipozungumza na timu ya wataalamu wa halmashauri (CMT) ya wilaya ya Mkinga, inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji (DED), Rashid Gembe.
Kwenye kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Katibu Tawala Wilaya (DAS), Salum Palango, Mnyema amesema kushindwa kutii na kutekeleza maelekezo ya mamlaka, ni kinyume cha kanuni za utumishi wa umma na kunafifisha utendaji kazi wenye matokeo chanya kwenye jamii.
Amesema, akiwa Msimamizi Mkuu wa watumishi wa umma mkoani humo, hatakuwa tayari kuona hali hiyo inajitokeza, na kwamba atakayejaribu kushiriki ukiukwaji huo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
‘’Anayedhani anaweza ku-test (kujaribu) mamlaka yangu, afanye hivyo kwa kukiuka maelezo yanayotolewa,’’ ameonya na kusema, utii wa maelekezo ni sehemu muhimu ya kudumisha nidhamu kazini.
Amesema, vitendo vinavyoathiri utendaji kazi kwenye halmashauri za wilaya, vinatoa ishara kwa watumishi husika kuhujumu lengo la kufanikisha mipango na miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Mkurugenzi wa halmashauri husika.
Mnyema, amewataka watumishi wa umma kwenye halmashauri na taasisi nyingine, kutafakari kuhusu mikata ya ajira zao iliyowapa majukumu wanayopaswa kuyatekeleza kwa weledi na uadilifu, ili kubadilisha hali iliyo mbaya kuwa yenye manufaa kwa wananchi.
AWAREJESHA MKINGA WATUMISHI WANAOISHI JIJINI TANGA
Mnyema amesema miongoni mwa mambo yanayokwamisha ufanisi na utoaji huduma bora kwa wananchi, ni hatua ya baadhi ya watumishi wa umma kuishi nje ya maeneo yao ya kazi.
Mnyema ametoa mfano kuwa wapo baadhi ya watumishi wa ngazi tofauti katika halmashauri ya wilaya ya Mkinga wanaoishi jijini Tanga, na amewaagiza kurejea na kuishi Mkinga ifikapo Januari 31, 2024.
Amesema agizo hilo linapaswa kutekelezwa kwenye halmashauri zote za mkoani Tanga, likisimamiwa na Makatibu Tawala Wilaya
Miongoni mwa wajumbe wa CMT walioshiriki kikao hicho wakathibitisha kuwa miongoni mwa wanaoishi jijini Tanga, hivyo kulipokea agizo la Mnyema na kukubali kuwa mabalozi watakaowaongoza watumishi wengine wa halmashauri hiyo kuweka makazi yao Mkinga.
DAS NAYE ATOA YA MOYONI
Naye DAS Palango ameunga mkono maelekezo ya RAS Mnyema na kusema, halmashauri ya Mkinga ina viashiria vya kuwepo baadhi ya watumishi wanaojihusisha na matendo yenye kutoa taswira ya kumkwamisha Mkurugenzi kutekeleza wajibu wake.
Hata hivyo, amesema hatua kadhaa zimekuwa zikichukuliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji Gembe.
DED: NITAENDELEA KUDHIBITI UZEMBE
Kwa upande wake, DED Gembe amesema uongozi wake umekuwa ukifuatilia mienendo ya watumishi, hali inayoendelea siku kwa siku na kwamba hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa maagizo ya RAS Mnyema.
Amesema ushiriki na ufuatiliaji wa ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, umekuwa msaada mkubwa wa kufanikisha mipango ya maboresho yanayowalenga watumishi wa umma katika utendaji kazi na utoaji huduma bora kwa jamii.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.