MKOA wa Tanga umenufaika kwa kupata mitungi ya gesi 26,040 yenye thamani ya Shilingi milioni 455.7, ikiwa na ujazo wa kilo sita kila mmoja..
Mitungi hiyo itakayouzwa kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 17,500, imetolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na itasambazwa na mtoa huduma, kampuni ya Manjis Logistic Limited.
Mpango huo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024 - 2034, utahusisha maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji kwenye wilaya nane za mkoa wa Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, ameiomba REA kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kila wakati, na kuwafikia wananchi kadri itakavyohitajika.
Mhe Balozi Dk Batilda amesema, hatua hiyo itawezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kuwa endelevu.
Pia, amesema Tanga inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi, huku akiwapongeza wadau mbalimbali wanaosaidia utekelezaji wa mpango huo, ikiwemo kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi.
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaoitumia ifikapo 2034,, ulizinduliwa Mei 8, 2024 na Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam.
Kabla ya uzinduzi huo, Mhe Rais Dk Samia, aliongoza mkakati kwa nchi za Afrika, kuwawezesha wanawake barani humu kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, wakati aliposhiriki Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) huko Dubai.
Shirika la Utangazaji za Deutsche Welle (DW) la Ujerumani lilipoti Mei 8, 2024 kuwa, ndani ya mkakati huo ambao ni wa miaka 10, Mhe Rais Dk Samia, anataka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza chachu kufikia malengo yake.
DW iliripoti kuwa, ikiwa sehemu ya kushajiisha uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, kada mbalimbali ya watu walihudhuria wakiwamo viongozi wa kisiasa, kidini, wanadiplomasia na makundi mengine kama vile madereva wa malori, mamalishe na vikundi vya wanawake ambao wanatajwa kuwa sehemu kubwa ya matumizi ya nishati isiyo rafiki.
Kwa mujibu wa DW, zaidi ya asilimia 90 ya kaya nchini Tanzania hutegemea nishati chafu itokanayo na kuni, mkaa pamoja na mabaki ya kinyesi cha wanyama, kwa ajili ya kupikia na shughuli nyingine za majumbani, hali ambayo wataalamu wanaonya kwamba imekuwa sehemu ya ongezeko la matatizo ya kiafya, huku pia uharibifu wa mazingira ukivunja rekodi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa akasema kwenye hafla hiyo kuwa Serikali imeanisha vipaumbele vitakavyozingatiwa kuanzia ngazi ya kaya mpaka taifa.
DW ikaandika kuwa, ripoti zinaonyesha kwamba kila mwaka hapa nchini, watu 33,000 hupoteza maisha kutokana na mikasa inayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama, na kiwango hicho kinadhihirika zaidi kwenye maeneo ya vijijini ambako uwepo wa nishati safi na salama ya kupikia bado ni ndogo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.