Na Emma Kigombe, OMM TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amewataka vijana kuibua mawazo chanya yenye ubunifu, yatakayowanufaisha kutokana na fursa mbalimbali kwenye jamii na soko la kimataifa.
Mhe Balozi Dk Batilda, ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa mtandao wa fursa kimataifa na jukwaa la vijana, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Tanga International jijini Tanga na kuratibiwa na mradi wa Tanga Yetu.
Amesema majukwaa ya vijana yanatoa nafasi kwao (vijana) kujadili masuala muhimu yanayowakabili, ikiwemo upatikanaji wa fursa za ajira, elimu na nyanja nyingine za maendeleo.
Pia, Mhe Balozi Dk Batilda amesema majukwaa hayo yanawezesha wadau mbalimbali kuonesha na kujadili fursa zinazopatikana kwa vijana ikiwa ni pamoja na bidhaa wanazozalisha na kukuza ubunifu wao.
“Uzinduzi wa majukwaa haya ya vijana ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa vijana wanapata nafasi ya kujitokeza, kutoa mawazo yao na kutangaza bidhaa na huduma wanazozalisha. Hii ni fursa ya kuonyesha ubunifu na kupata msaada katika kuzifikisha biashara zao kwenye soko pana,” amesisitiza Mhe Balozi Dk Batilda.
Mhe Balozi Dk Batilda, ametoa wito kwa vijana mkoani humo kutumia jukwaa hilo kutangaza na kushirikiana na wadau wengine, ili kujenga mtandao wa biashara na ufundi, utakaowanufaisha katika sekta mbalimbali.
Nao vijana kutoka maeneo tofauti ya mkoani Tanga, wameelezea kuridhishwa kwao na ishara za upendo na kujali maslahi yao, kunakofanywa na Mhe Balozi Dk Batilda.
Hadija Athuman Amiri anayefanya kazi katika taasisi ya Health and Economic Driver iliyopo ya Muheza, anasema vijana wanapaswa kuondokana na woga katika kuanzisha biashara na huduma zinazotokana na mawazo bunifu waliyonayo.
Anasema, viongozi wa Serikali, akitolea mfano wa Mhe Balozi Dk Batilda, wanaonyesha utashi wa kuwasaidia na kuwawezesha vijana kukabiliana na changamoto walionazo, hivyo ipo haja kwao (vijana) kuwa wabunifu na wenye ujasiri katika kutekeleza mipango yao.
Naye Abdul Seleman anayeendesha bajaji wilayani Pangani, amesema wepesi wa kuibua wazo bunifu kwa vijana unategemea zaidi ubobezi wao kwenye shughuli wanazozifanya kwa weledi na ufanisi.
‘’Ukiibua wazo bunifu linalolenga kufanya biashara, huduma ama shughuli yoyote ambayo kijana anaijua vizuri, inakuwa rahisi kutekeleza, kusimamia na kutathmini mafanikio,’’ anasema.
Kwa upande wake, Charles Mgoghwe anayejishughulisha na masuala mbalimbali kwenye tasnia za siasa na maendeleo ya vijana wilayani Muheza, anasema changamoto za kijamii na mazingira ni miongoni mwa vyanzo kwa vijana, kuibua mawazo bunifu katika kuzikabili.
‘’Kama kuna changamoto inaikabili jamii ama katika masuala ya mazingira, ni wazi kwamba vijana tunapaswa kuibua mawazo bunifu yanayotoa majawabu ya kuzikabili (changamoto) husika,’’ anasema.
Mgoghwe anaongeza kuwa, utekelezaji wa mawazo bunifu unapaswa kutegemea zaidi uwezo wa rasilimali kama fedha alionao kijana, mahitaji na ushindani kwenye soko la bidhaa ama huduma.
Anatoa mfano, mabadiliko ya tabia nchi yaliyopo, yanaweza kuwa fursa kwa vijana kubuni miaradi ya vitalu vya miti kwenye maeneo yao, hasa yaliyopo kandoni mwa barabara na yale ya wazi, ili kuwawezesha wateja wengi kuwafikia.
Kwa ujumla, vijana hao wamempongeza Mhe Rais Dk Samia Suluhu kwa kuwa kinara wa kuwahimiza (vijana) kuibua mawazo bunifu, yakiwemo yaliyosababisha kuanzishwa kwa programu mbalimbali zinazolenga maendeleo ya vijana nchini, ikiwemo mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.