Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
RAIS Mhe Dk Samia Suluhu Hassan, ‘amewashika mkono’ wazee, na watoto yatima wanaolelewa kwenye vituo vitatu vya malezi jijini Tanga, ili washiriki sikukuu ya mwaka mpya wa 2025 kwa furaha zaidi.
Zawadi hizo zimetolewa leo Desemba 30, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, kwa niaba ya Mhe Rais Dk Samia kwenye Kituo cha Malezi ya Wazee Mwanzange kinachomilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mhe Balozi Dk Batilda, alikabidhi zawadi hizo kwa wazee wa kituo hicho na watoto yatima 25 wanaolelewa kwenye vituo vya Goodwill and Human na 78 waliopo kwenye Nyumba ya Furaha maarufu kama Casadellagioia cha Kanisa Katoliki.
Mhe Balozi Dk Batilda amesema Mhe Rais Dk Samia anaguswa na maisha ya kila Mtanzania, na hivyo kuwa sababu ya kufanya majitoleo yake kwa watu wanaoishi kwenye maeneo yenye uhitaji vikiwemo vituo hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya walezi wenzake, Sista Irene Yohana wa Kituo cha Nyumba ya Furaha, amesema ni jambo la faraja kwa Mhe Rais Dk Samia kuguswa na maisha ya wahitaji, wakiwemo watoto yatima wanaowalea kwenye vituo hivyo, na kwamba Mwenyezi Mungu amjalie na kumuongezea nguvu zaidi za kuusambaza upendo huo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Goodwill and Humanity, Muhdhar Hidarufi, pamoja na mambo mengine amesema, furaha ya watoto yatima na wazee wasiojiweza katika mwaka mpya 2025, ni ishara ya namna Mhe Rais Dk Samia anavyowajali Watanzania pasipo ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema, huduma zinazotolewa kituoni hapo ni pamoja na ushauri wa kisaikolojia ili kuimarisha na kukuza ukuaji chanya, ustawi na afya ya akili, elimu ya afya, usafi, lishe, na mahitaji ya msingi kama mavazi, chakula na malazi.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.