Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
MIONGONI mwa sifa za kale za mkoa wa Tanga ni kuwepo viwanda vya usindikaji na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, uliochangia ajira, uchumi na kipato kwa wakazi wake.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti, viwanda hivyo vilishindwa kufanya kazi hadi Serikali ilipochukua hatua ya kuondokana na hali hiyo, ikiwemo kuvibinafsisha kwa wawekezaji wengine.
Hatua hiyo iliwezesha baadhi ya viwanda kuibuka upya na kuzalisha katika hali inayokidhi malengo ya awali ya uanzishwaji wake, na vingine vimeendelea kutoweka huku wawekezaji wasioneshe ishara za kuvifufua na kuviendeleza.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, leo Desemba 31,2024 amezungumza kwenye ibada ya kumuombea dua Mhe Rais Samia Suluhu Hassan na Tanzania kwa ujumla, ambapo pamoja na mambo mengine, amegusia suala ya ‘kufa’ kwa baadhi ya viwanda vya mkoani humo.
Amesema, sababu za awali za ‘kufa’ kwa viwanda vingi ilihusiana na kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki Julai 1977, ikiwa ni takribani miaka 10 tangu kuasisiwa kwake 1967. Jumuiya hiyo iliundwa tena upya Julai, 2000.
Mhe Balozi Dk Batilda anasema, kutokana na kuwepo viwanda visivyoendelezwa kama ilivyokusudiwa na Serikali, uongozi wa mkoa wa Tanga unawafuatilia wawekezaji, ili viendelezwe na watakaoshindwa, hatua za kuvirejesha zichukuliwe.
KURITHISHA KAZI ZA MIKONO
Pamoja na nafasi ya viwanda katika kutengeneza ajira na ukuzaji uchumi, Mhe Balozi Dk Batilda amewahimiza wazazi na walezi, kuwarithisha watoto wao ‘kazi za mikono’, ili watengeneze bidhaa za asili na kitamaduni zilizohitajika kwenye masoko ya ndani na nje.
AITAJA MIRADI YA MABILIONI YA RAIS SAMIA
Mhe Balozi Dk Batilda amesema, Tanga imenufaika kwa kiasi kikubwa na fedha nyingi zinazotolewa na Mhe Rais Samia, kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wakazi wake.
Ameitaja baadhi ya miradi hiyo ni uboreshwaji wa bandari ya Tanga uliogharimu Sh bilioni 429.1, ujenzi wa vituo vya huduma za afya kama vile zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Ametoa mfano kuwa, baada ya maboresho yaliyofanyika, hivi sasa bandari ya Tanga inapokea meli kubwa 35 zinazotoka moja kwa moja nje ya nchi, ikilinganishwa na meli 18 za awali kwa kipindi cha mwezi mmoja pekee.
Kwa hesabu hiyo, Mhe Balozi Dk Batilda amesema kwa kipindi cha miezi mitano ya kufikia Novemba, 2024, bandari hiyo ilipokea jumla ya meli 172, huku kukiwa na ajira 16,000 kwa Watanzania, ilinganishwa na 4,000 za awali.
Mhe Balozi Dk Batilda anasema, kwa maboresho hayo yaliyohusisha ununuzi na matumizi ya mashine bora za kupakia na kupakua, hivi sasa mizigo inachukua kati ya siku tatu hadi tano kushushwa na kusafirishwa.
Miradi mingine ni Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, ujenzi wa shule za msingi na sekondari, maabara na maktaba za shule hizo, vituo vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Katibu wa Siasa, Mafunzo na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, Mngazija, amesema dua kwa viongozi wa nchi hususani Mhe Rais Samia ni jambo linalochochea utulivu, amani na maendeleo kwa Taifa.
Kwa hali hiyo, Mngezija amesema hatua iliyofikiwa na Mhe Balozi Dk Batilda kuandaa dua hiyo ni yenye kupongezwa.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.