Na Nassoro Rashid, MKINGA
KASI ya vita ya udhibiti wa dawa za kulevya mkoani Tanga, inaongezeka, viongozi wakiiasa jamii ishiriki kikamilifu kuondokana na hali hiyo.
Takribani siku 20 baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali, Mwantumu Mahiza, kuhimiza udhibiti zaidi dawa za kulevya mkoani Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe Gilbert Kalima, ‘ameipita njia hiyo’ wakati akizindua jengo la Kamati za Usimamizi wa Eneo la Pamoja la Uvuvi (CFMA).
Mhe Kalima, ameiasa jamii kushirikiana na Serikali, kupiga vita dawa za kulevya zinazochangia kushamiri kwa mmomonyoko wa maadili ukiwemo ukatili na ubakaji.
Ameyasema hayo jana Agosti 26, 2025 katika kijiji cha Mwaboza, kata ya Moa baada ya kuzindua jengo hilo la Mtandao wa Jamii za Ufukweni Mwambao, kwa ufadhili wa Shirika la Iconic la Marekani.
Mhe Kalima ameishukuru Iconic kwa kufanikisha ujenzi wa jengo hilo lililogharimu Shilingi milioni 69, na ameahidi Serikali italisimamia na kuhakikisha linatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Pia, Mhe Kalima amesema ipo haja ya kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za pwani na baharini, kwa kuvishirikisha vikundi vya hifadhi ya mazingira, uzuiaji uvuvi haramu, usafirishaji wa dawa za kulevya na migogoro inayoleta mafarakano kwenye jamii.
Aidha, amesema Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, inajenga Soko la Samaki Moa, hivyo juhudi hizo hazitakuwa na tija endapo mazingira ya bahari hayatatunzwa.
Ametoa rai kwa vijiji tisa vilivyohusika kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha mazalia ya samaki yanabaki salama kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mhe Kalima amewataka wakulima wa mwani kushirikiana na Vikundi vya Ulinzi na Usimamizi wa Mazingira ya Bahari (BMU) ili kilimo hicho kisisababishe migongano na shughuli za uvuvi.
Ujenzi wa jengo hilo lenye Ofisi za Mtendaji wa Kijiji na Kamati ya Usimamizi, vyoo viwili vya kisasa, ukumbi wa mikutano, chumba cha kukodishwa, kisima na samani, ulianza Machi 2025 na kukamilika Agosti 2025.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.