Na Emma Kigombe, OMM TANGA
SERIKALI inakusudia kujengwa viwanda vipya 9,048 vitakavyotoa ajira zaidi ya milioni 6.5 ifikapo 2030.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Dkt Selemani Jafo, ameyasema hayo jana Agosti 20, 2025, alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Chama cha Maafisa Biashara Wanawake Tanzania (TAWTO), unaofanyika mkoani Tanga.
Amesema ujenzi wa viwanda hivyo ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta hiyo muhimu kwa ukuzaji wa teknolojia, uzalishaji na ajira.
Mhe Dkt Jafo amesema dhamira ya Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji nchini, na kuongeza uzalishaji wa viwandani.
Kwa mujibu wa Jafo, Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaboreshwa na viwanda vipya vinaanzishwa kwenye maeneo mbalimbali, ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, Mhe Dkt Jafo amesema Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inatatua changamoto zinazowakabili Maafisa Biashara nchini, ikiwemo uhaba wa vitendea kazi.
Alisisitiza kuwa kundi hilo halipaswi kubezwa, kwani linachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
“Ni lazima tuwape thamani stahiki Maafisa Biashara. Hawa si ‘spare tyre’ (tairi ya ziada) bali ni sehemu muhimu ya maendeleo ya uchumi wetu,” akasema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amesema pamoja na changamoto za kiuchumi zilizowahi kusababisha kufungwa kwa baadhi ya viwanda mkoani humo, juhudi za kuvifufua zimeanza kuzaa matunda.
Mhe Balozi Dkt Batilda, amesema Tanga imejipanga kuanzisha viwanda vipya vikiwemo vya magari ya wagonjwa na vya kusindika samaki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWTO, Elizabeth Swagi, alisema chama hicho kitaendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo kwa kuwapatia elimu ya sheria, miongozo na taratibu za biashara ili washiriki ipasavyo katika uchumi wa taifa.
Mkutano Mkuu wa Nne wa Chama cha Maafisa Biashara Wanawake Tanzania (TAWTO) una kaulimbiu mbiu inayosema, “Mwanamke Mpambanaji ni Nguzo ya Maendeleo ,Tushiriki Vyema Uchaguzi Oktoba.”
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.