Na Mashaka Mgeta, MKINGA
NI kama kusema, ‘’samaki mkunje, angali mbichi.’’ Ndivyo historia inavyoandikwa leo Desemba 11, 2024 kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, kufungua mafunzo elekezi kwa Wenyeviti wa Vijiji 85 vilivyopo wilayani Mkinga mkoa wa Tanga.
Wenyeviti hao walioshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024 wametokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama ilivyokuwa kwa Wenyeviti wa Vitongoji 332 kati ya 335 walioshinda kutokea chama hicho, huku viti vitatu vikichukuliwa na wagombea kupitia Chama Cha Wananchi (CUF).
Akifungua mafunzo hayo kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Mkinga, Mhe Balozi Dk Batilda akajikita kwenye maeneo nane yenye kutoa dira kwa viongozi hao, kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika ngazi ya kijiji.
MOSI: KUTANGAZA MAFANIKIO YA RAIS SAMIA SULUHU
Mhe Balozi Dk Batilda amesema, miongoni mwa hoja zilizotumika kuwashawishi wapiga kura hadi kuwachagua Wenyeviti wa Vijiji hao, ni mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa ahadi za Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ikiwemo miradi mikubwa katika sekta za maji, afya, miundombinu, elimu, kilimo, barabara na huduma mbalimbali za kijamii.
Amesema, kwa vile utekelezaji wa ahadi hizo unaendelea, viongozi hao wanapaswa ‘kuyabeba’ mafanikio hayo na kuyashirikisha kwa kina kwa wananchi kwenye maeneo yao, ili wayasikie na kuyaona.
PILI: USALAMA, AMANI NA UTULIVU
Mhe Balozi Dk Batilda amesema, viongozi hao wanapaswa kuimarisha usalama, amani na utulivu, ili kufanikisha jukumu msingi la Serikali kwenye maeneo yote, kuwashirikisha wananchi kujenga mahusiano mazuri ya kuwafanya kutoa taarifa kwao (wenyeviti wa vijiji) na vyombo vya ulinzi na usalama.
‘’Wote ni mashaidi kuwa, sehemu yoyote ambayo haina amani na utulivu, wananchi hawatakuwa na muda wa kushiriki shughuli za maendeleo, hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi, mshikamano na maendeleo ya jamii,’’ amesema.
TATU: MAPATO YA NDANI
Mhe Balozi Dk Batilda amewaagiza Wenyeviti wa Vijiji hao, kusimamia mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ilivyo kipaumbele cha Serikali.
Amesema, Serikali inasisitiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato hayo, kwa vile imeonesha mafanikio katika kudhibiti mianya ya upotevu hususani kutokana na watumishi wasio waaminifu.
Pia amesema mifumo hiyo inarahisisha upatikanaji wa taarifa za vyanzo mbalimbali vya mapato yaliyokusanywa kwa kipindi husika, na kusaidia kuongezeka kila mwaka.
Hali hiyo, kwa mujibu wa Mhe Balozi Dk Batilda, inawezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu, kupitia ruzuku na wafadhili wa nje.
Mhe Balozi Dk Batilda amesema, Wenyeviti wa Vijiji wanapaswa kutekeleza wajibu huo kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Vitongoji, Madiwani) na Watendaji wa Vijiji.
NNE: KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO
Mhe Balozi Dk Batilda amesema Serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi wa Mhe Rais Dk Samia, imetoa fedha nyingi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa vituo vya afya, madarasa na mabweni kwa kutumia mfumo wa ‘’force account’’ wenye manufaa ya kutumia fedha kidogo kwa kazi kubwa.
Hata hivyo amesema, yapo maeneo yaliyofanya vizuri kupitia utaratibu huo, na mengine, utekelezaji wake unakabiliwa na changamoto zinazotokana na usimamizi hafifu, hali inayosababisha kukamilishwa kwa miradi ikiwa chini ya viwango, na kukosa thamani ya fedha.
‘’Hivyo, nasisitiza mkafuatilie na kusimamia vizuri fedha za miradi inayoletwa na Serikali katika maneo yenu, ili fedha hizo zilete matokeo tarajiwa na kuwaondolea wananchi changamoto za kukosa huduma,’’ ameagiza.
TANO: KUIMARISHA UADILIFU
Mhe Balozi Dk Batilda amesema, hatua waliyofikia Wenyeviti wa Vijiji hao ni mfano wa kuwa watumishi wa umma, hivyo wana wajibu wa kutoa huduma bora kwa wananchi, na kwa kuzingatia misingi, kanuni na desturi za uadilifu.
‘’Mnapaswa kufahamu vema na kuzingatia kanuni za maadili, kutumia misingi ya haki badala ya upendeleo pale mnapotoa huduma kwa wananchi, kuweka vizuri malengo halisi ya kazi zenu ili kuwawezesha kufikia kiwango cha juu katika utendaji wenu wa kazi,’’ Mhe Balozi Dk Batilda ameasa.
Vilevile, Mhe Balozi Dk Batilda amewaagiza viongozi hao kudumisha mahusianao mazuri mahali pa kazi, na kwa wananchi watakaowafikia kupata huduma hususani kwenye ofisi za umma.
SITA: KERO NA MALALAMIKO
Mhe Balozi Dk Batilda amesema miongoni mwa mambo ya msingi kwa Wenyeviti wa Vijiji hao ni kutatua kero na malalamiko ya wananchi, vinginevyo, wananchi wataonesha kutoridhishwa na huduma za uongozi wao.
SABA: USHIRIKISHWAJI WANANCHI
Mhe Balozi Dk Batilda amewaagiza viongozi hao kuondokana na kasumba ya kutoitisha vikao na mikutano ya wananchi kwenye vijiji na vitongoji, hali inayowanyima wananchi haki ya kikatiba ya kupata taarifa, na kushirikishwa kwenye maamuzi yanayohusu maisha yao.
NANE: KUPIGA VITA UKATILI, UNYANYASAJI NA DHULUMA
Mhe Balozi Dk Batilda amesema, jamii inakabiliwa na ongezeko la vitendo vya ukatili vikiwemo unyanyasaji na dhuluma hasa kwa wanawake na watoto, hivyo ni wajibu wa viongozi hao kuhakikisha kunakuwepo udhibiti na kuvizuia kwenye maeneo yao.
Amesema utekelezaji wa agizo hilo unapaswa kuwahusisha watu kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, yakiwemo yanayotajwa kuwa sehemu ya vyanzo vya vitendo hivyo kama vile waganga wa tiba asilia wasiokuwa waaminifu kwa kazi zao.
MKUU WA WILAYA AWATAKA WAUHESHIMU UENYEKITI
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe Gilbert Kalima, amewaasa Wenyeviti wa Vijiji hao kuiheshimu nafasi hiyo waliokabidhiwa na wananchi, na kwamba mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha kufanya kazi vizuri zaidi na kukidhi thamani na hadhi ya nafasi hiyo katika uongozi.
Mhe Kalima amesema, mafunzo hayo yamepangwa kwa awamu tofauti wilayani humo, ambapo pia yatawahusisha wajumbe wa halmashauri za serikali za vijiji, ili kuunganisha mnyororo wa ufahamu wa pamoja kutoka ngazi ya wilaya, halmashauri, tarafa, kata, kijiji na kitongoji.
Amezitaja mada tisa zilizowasilishwa kwenye mafunzo hayo kuwa ni taratibu za uendeshaji wa vijiji, wajibu wa viongozi wa serikali za mitaa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya na uhamiaji haramu, usajili wa raia, udhibiti wa migogoro ya ardhi na itifaki za viongozi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mhe Amani Kasinya amewataka viongozi hao kushirikiana na wananchi kukomesha vitendo viovu, vikiwemo vya mahusiano ya watu wa jinsi moja, kwa vile vinaashiria pia machukizo kwa Mwenyezi Mungu.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.