Na Mashaka Mgeta, MTWARA
BAADA ya takribani miaka 42 na miezi miwili ya kuishi duniani kutamatika, aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Selemani Sankwa, jana Desemba 22, 2024, amezikwa kwenye makaburi ya Msafa yaliyopo mtaa na kata ya Tandika, manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Kwa mujibu wa wasifu uliosomwa na Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Tanga, Samwel Mngazija, Sankwa aliyezaliwa, Oktoba 19, 1982 alifariki Desemba 20, 2024 kutokana na maradhi ya moyo, shinikizo la damu, sukari na kiharusi.
Kabla ya kwenda kuzikwa, mwili wa marehemu Sankwa umeswaliwa nyumbani kwake mtaa wa Magomeni A, kata ya Magomeni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali walioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Mongella.
Viongozi wengine ni pamoja na Wakuu wa Mikoa, Mhe Balozi Dk Batilda Burian (Tanga) na Mhe Kanali Patrick Sawala (Mtwara), Wenyeviti wa Mkoa wa CCM, Rajab Abdallah (Tanga), Thomas Ole Sabaya (Arusha) na Said Nyengedi (Mtwara).
Pia walikuwepo wajumbe wa kamati za siasa za wilaya na mikoa za Mtwara, Lindi na Arusha na wawakilishi wa wabunge wa Tanga na Mtwara, viongozi wa serikali na wakazi wa Mtwara.
MONGELLA: ALIKUWA MFANO WA VIONGOZI BORA
Akizungumza kabla ya mazishi, Mongella amesema uwezo na karama za uongozi za Sankwa, ni miongoni mwa ishara hai za mafanikio ya mpango wa CCM, kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora.
Hata hivyo, Mongella amesema ni kazi ngumu kwa taasisi kama chama cha siasa, ‘kuwatengeneza’ viongozi wenye uwezo wa aina ya Sankwa.
‘’Ni vigumu sana kuwatengeneza viongozi wa aina ya Sankwa,’’ amesema na kufichua kwamba CCM, kwa kutambua vipaji na karama zake za uongozi, ilishaanzisha mchakato wa kumhamishia Makao Makuu jijini Dodoma kwa kazi kubwa zaidi.
Mongella amesema uasili huo unaopata uungwaji mkono wa umma, kuheshimiana, kuthaminiana na maombi ya viongozi wa dini, vinasababisha ugumu kwa chama hicho kuharibikiwa.
Amesema Sankwa alitokea kwenye ‘mizizi’ ya CCM, akawa mtumishi wa umma katika sekta ya elimu na baadaye kurejea kukitumikia chama hicho katika nafasi tofauti hadi kufikia Katibu wa Mkoa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
RAJABU: ALIPENDA USHIRIKIANO, HAKUWA NA MAKASIRIKO
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Rajabu amesema Sankwa aliuishi na kueneza ushirikiano, kutokuwa na makasiriko, hali iliyozidi kukiimarisha chama hicho mkoani Tanga.
‘’Ukituuliza sisi watu wa Tanga kuhusu mabaya ya Sankwa hautayawapata kwa sababu hatujayaona, hivyo hatuyajui, japo tunatambua kila binadamu ana udhaifu wake. Isipokuwa mazuri yake kwetu yapo tele na kama ni kuyaelezea yote, muda hautatosha,’’ amesema.
Rajabu amewahimiza watu kumuomba Mungu awajalie neema za kutenda mema duniani, ili mwisho wa maisha ukifika, makaburi yao yawe bustani ya peponi badala ya kuwa shimo la motoni.
BALOZI BATILDA: AMECHANGIA MAFANIKIO YA CCM TANGA
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Burian, amesema ufanisi wa kazi wa Sankwa, umechangia kuifanya CCM izidi kuaminika, na kukiwezesha kupata ushindi wa asilimia 99.88 kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 27,2024.
Mhe Balozi Dk Batilda, amesema akiwa mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa (CCM), ameshuhudia zaidi vipaji na umahiri wa uongozi wa Sankwa ikiwa ni pamoja na wepesi wa kuomba msamaha na kujisahihisha anapoamini amekosea.
ARUSHA WAMTAJA KWA UFASINI KAZINI
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Ole Sabaya, akasema mafungamano ya kisiasa yanayotokana na Mwenyekiti wa Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Rajabu kuwa mlezi wa CCM Arusha, ndipo walipomjua na kutambua umahiri wa uongozi wa Sankwa.
Amesema, wakati wa uhai wake, Sankwa alitekeleza kwa ufanisi maelekezo ya Mwenyekiti wake yaliyoimarisha mahusiano ya kisiasa na kijamii kati ya mikoa miwili hiyo.
HISTORIA YAKE
Sankwa alizaliwa Oktoba 10, 1982 mkoani Mtwara na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Ziwani kati ya 1989 na 1995.
Mwaka 1996 – 1999, Sankwa alipata elimu katika Shule ya Sekondari alipohitimu kidato na nne.
Mwaka 2017 hadi 2022, Sankwa alisomea Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu Huria (OUT), mwaka 2013 hadi 2016 alisomea Stashahada ya Elimu chuoni hapo na 2000-2002 alisomea Astashahada ya Elimu Daraja A katika Chuo cha Ualimu Mtwara.
MAFUNZO
Sankwa alipata mafunzo na semina mbalimbali ya uongozi na ujasiriamali katika chama na jumuiya zake.
AJIRA
Kabla ya kuajiriwa na CCM alishika nafasi za Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Mtwara Vijijini (2017 – 2019), Katibu wa Hamasa UVCCM wilaya ya Mtwara Vijijini (2008 – 2012), Katibu wa Siasa na Uenezi wa Wilaya ya Mtwara, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Mtwara.
SERIKALINI
Sankwa amewahi kuwa mtumishi wa umma ambapo mwaka 2019, alikuwa Mratibu Elimu Kata ya Mahurunga, Mratibu Kata ya Msanga Mkuu (2013 – 2019), Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Namtumbuka (2010 – 2011) na Mwalimu Shule ya Msingi Mtwara Vijijini (2003 – 2010).
KUAJIRIWA CCM
Sankwa aliajiriwa na CCM Machi 30, 2023 katika wadhifa wa Katibu wa Wilaya ya Tanga Mjini na Agosti 16, 2023 aliteuliwa kuwa Kaimu Katibu wa CCM wa Mkoa wa Tanga.
Inalillah Wainalillah Rajiun
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.