Na Mashaka Mgeta, OMM – TANGA
KAMA ni miongoni mwa ‘wanaosugua akili’ kutafuta sababu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutong’ooka madarakani, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe Hemed Suleiman Abdulla, ametegua kitendawili hicho leo Agosti 17, 2024 jijini Tanga.
Mhe Abdulla ambaye pia ni Mlezi wa CCM wa mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye vikao vya ndani katika wilaya za Tanga na Mkinga mkoani humo.
Amesema, wakati vyama vikongwe vikiondolewa madarakani kwenye nchi mbalimbali hususani barani Afrika, CCM iliyoanzishwa Februari 5, 1977 kutokana na Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP), kinabaki madarakani kwa vile kinatekeleza Ilani ya Uchaguzi na ahadi zinazotolewa na viongozi wake.
Mhe Abdulla anasema kutokana na hali hiyo, CCM inazidi kuungwa mkono na Watanzania wengi wakiwamo wanaojiunga kutokea vyama vya upinzani.
Hivyo, Mhe Abdulla amewataka viongozi na wanachama wa CCM kujiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu wa 2025 huku akisisitiza umuhimu wa kufuata Katiba, Kanuni na Taratibu zinazowaongoza kuwapata wagombea katika ngazi zote.
Mhe Abdulla anasema, zipo taarifa za watu ‘wanaojipitisha’ kwenye maeneo ya uchaguzi wakiwa na dalili za kuwepo ‘watu nyuma yao’ wanaowaunga mkono, na ameonya kuwa Chama hicho hakiwezi kuivumulia hali hiyo.
Amesema viongozi wa CCM katika wanapaswa kuendeleza ustaarabu na heshima ya chama hicho kwa kufuata taratibu zake kuhusu viongozi wa kuchaguliwa na wananchi, hali itakayoimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao.
Kwa mujibu wa Mhe Abdulla, hatua ya kwenda kinyume cha Katiba, Kanuni na Taratibu za CCM ni sawa na kukihujumu chama hicho kinachoendelea kupendwa na kuungwa mkono na Watanzania wengi zaidi.
Hata hivyo, Mhe Abdulla amesema CCM haiwezi ‘kuwabeba’ viongozi waliochaguliwa, lakini wakashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
‘’Ninawasihi viongozi wenzangu, tusiwe tayari kubeba mizigo isiyobebeka, kwa viongozi wanaotekeleza majukumu yao ipasavyo wasiwe na wasiwasi, tutakwenda nao, lakini wale walioshindwa, tutawaacha tu,’’ amesema.
Naye Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama hicho, Rajabu Abdallah, amesema wapo viongozi hususani wenyeviti wa vijiji, wanaoichonganisha CCM na wananchi kupitia ushiriki wao kwenye migogoro ikiwemo inayohusiana na ardhi, na kwamba hatakuwa tayari kuwaunga mkono.
‘’Wenyeviti wa aina hiyo walio wachonganishi, wanaouza ardhi kiholela na kusababisha migogoro, sipo tayari kuwanga mkono…watasafishwa kwa sabuni gani,’’ amesema na kuhoji.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.