Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe Hemed Suleiman Abdulla, amewaelekeza watendaji serikalini na katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tanga, kufanya kazi, ili kufanikisha matamanio ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania.
Mhe Abdulla ambaye pia ni Mlezi wa CCM wa Mkoa wa Tanga amesema, matarajio ya Mhe Rais Dk Samia ni kwa utawala wake kushughulikia mahitaji ya Watanzania, ili kwa pamoja, taifa lipige hatua kubwa za maendeleo na ustawi wa jamii.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, aliyewasili leo Agosti 16, 2024 katika ziara ya siku sita mkoani humu, amesema utendaji kazi wenye tija kwa watumishi hao, utaharakisha utekelezaji wa ahadi za Mhe Rais Dk Samia na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/2025.
Mhe Abdulla amesema hali hiyo inaweka mazingira bora ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani kuwa wenye ushindi mkubwa usiotumia nguvu kubwa kuyanadi mafanikio ya utawala wa Mhe Rais Dk Samia.
…AWAKEMEA WANAOJIPITISHA
Mhe Abdulla amewaonya wanasiasa wanaojipitisha kwenye maeneo ya uchaguzi kabla ya wakati, hali inayozua hofu kwa viongozi wa kuchaguliwa na wananchi waliopo madarakani sasa.
Amesema, chama hicho kinafuatilia kwa karibu wahusika wa kadhia hiyo na kwamba, watakaobainika watafikishwa kwenye kamati ya maadili za chama hicho.
Hata hivyo, Mhe Abdulla, amewataka viongozi na wawakilishi wa wananchi walioshinda kwenye chaguzi zilizopita, kufanya kazi kwa kujiamini, lakini kutambua pia kuwa, nyadhifa za kuchaguliwa hazina hatimiliki ya mtu mmoja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amesema hali ya kisiasa mkoani humo ni ya utulivu, huku kukishuhudiwa fedha nyingi zinazotolewa na Mhe Rais Dk Samia kwenye sekta mbalimbali za maendeleo.
Mhe Balozi Batilda ametoa mfano wa mafanikio hayo kuwa ni takribani Shilingi trilioni 2.7 zimetolewa katika kipindi cha utawala wa Mhe Rais Samia, huku trilioni 1 zikielekezwa kwenye sekta ya maji pekee.
Mwenyekiti wa Mkoa wa CCM, Rajabu Abdalla amesema kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao, vinagusa vipaumbele vyake mahususi wakati akiwania nafasi hiyo, alipoahidi kuhakikisha kuwa chama hicho kitaendelea kushika dola.
Awali, Katibu wa Mkoa wa CCM, Suleimani Sankwa, amesema chama hicho kinaendelea vema na mchakato wa uandikishaji wanachama kwa mifumo ya kielektroniki.
Pia Sankwa amesema CCM mkoa wa Tanga inaendea na utekelezaji wa miradi ya chama ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi wakena uboreshaji wa ofisi ya mkoa utakaogharimu Shilingi milioni 354.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.