Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi (BWZ), Mhe Zubeir Ali Maulid amegawa mitungi ya gesi 61 kwa wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii mkoani Tanga, ikiwa ni ishara ya kuadhimisha miaka 61 ya Muunganio ulioanzishwa Aprili 26, 1964.
Tukio hilo limefanyika Aprili 26, 2025 jijini Tanga kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara ya siku nne ya Mhe Maulid na maadhimisho ya miaka 61 yaliyohudhiriwa na wakazi wa mkoani humo.
Akizungumza baada ya kukabidhi mitungi hiyo, Mhe Maulid amesema Watanzania wana dhamana ya kuulinda, kuuenzi, kuuendeleza na kuihifadhi heshima inayotokana na uwepo wa Muungano.
Mhe Maulid amewaasa wakazi wa Tanga kujitokeza kwa wingi, kuwachagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kwa kuwa ndio njia muafaka ya kidemokrasia ya kuunda Serikali inayotokana na wananchi.
Amewaponza Mhe Rais Dkt Samia na Mhe Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar kwa kufanikisha miradi mbalimbali inayotatua kero za wananchi katika pande mbili za Muungano, na kuiasa jamii kuendelea kuwaunga mkono na kuwaombea mema.
Mhe Maulid amesema Muungano unapaswa kudumu kwa vile umetokana na dhamira ya viongozi waasisi (Nyerere na Karume) na waliofuata, unasimamia misingi na malengo ya uundwaji wake, umetokana na udugu wa kihistoria, umeleta umoja na mshikanano wa kitaifa kupitia matumizi lugha na sarafu moja, ulinzi na usalama vimeimarika.
“Hatuna budi kuyalinda na kuyaendeleza mafanikio ya Muungano kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo. Pia elimu kwa umma kuhusu Muungano iendelee kutolewa kwani ni muhimu na jukumu la wananchi wote,” amesema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Mkinga mkoani Tanga, Mhe Dustan Kitandula, amesema wakazi wa Tanga wanatambua, kuthamini na kuheshimu miradi mingi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika kipindi cha utawala wa Mhe Rais Dkt samia Suluhu hassan.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amesema Muungano ni sehemu ya zawadi kuu kwa nchi na raia wake, ukiwa umeasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Aman Karume walioweka maslahi binafsi pembeni na kuziunganisha Zanzibar na Tanganyika.
Amesema ni wajibu wa kila rai ana wote wenye mapenzi mema kuuenzi na kuudumisha, kwa vile kupitia Muungano huo, nchi imepiga hatua kubwa za maendeleo kwa pande zote za Muungano, akitoa mfano wa kila halmashauri kuwa na Hospitali ya Wilaya zinazochochea upatikanaji huduma bora za afya ambazo awali, zilitolewa kwenye hospitali za rufaa za mikoa.
Amewaasa wakazi wa Tanga kuendelea kuutafakari Muungano na mafanikio yake katika maeneo tofauti kama vile muingiliano wa watu binafsi na jamii za Zanzibar na Tanzania Bara.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdalla, amesema miradi inayotekelezwa inalenga kuwaondolea wananchi changamoto zinazowakabili, na kwamba miradi iliyotembelewa na Mhe Maulid ni sehemu ndogo ya miradi mingi katika miaka minne ya utawala wa Mhe Rais Dkt Samia.
Abdalla amesema kutokana na mafanikio yaliyopo, ni kiu ya wakazi wa Tanga kushiriki na kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 na ‘kumlipa deni’ Mhe Rais Dkt Samia, kuthamini umuhimu wa Muungano na kuendelea kuuenzi na kuyaendeleza maono halisi ya hayati Nyerere na hayati Karume.
Amesema, mafanikio yanayotokana na uongozi wa Mhe Rais Dkt Samia ni sehemu ya manufaa ya Muungano kama ilivyo kwa CCM iliyotokana na Afro Shiraz Party (ASP) ya Zanzibar na Tanganyika African National Union (TANU) ya Tanzania Bara.
Naye Mbunge wa zamani wa Pangani, Mhe Rished Abdallah amesema hatua kubwa za maendeleo zimefikiwa tofauti na kipindi cha Bunge la kwanza katika mfumo wa vyama vingi lililotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.
“Nikikumbuka mambo yalivyokuwa wakati ule na sasa, naona kama ni ndoto hai, hivyo ipo haja ya kuishukuru CCM kwa sera na siasa zake, kwa amani na utulivu vilivyopo nchini,” amesema.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.