Na Mashaka Mgeta, HANDENI
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), Mhe Zubeir Ali Maulid, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi, kushiriki na kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ili kupata viongozi watakaounda Serikali yenye kutekeleza miradi ya maendeleo na huduma za ustawi wa jamii.
Mhe Maulid ameyasema hayo leo Aprili 24, 2025 alipozungumza na wakazi wa Handeni, baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maabara ya Hospitali ya Wilaya iliyopo halmashauri ya Mji Handeni.
Ziara ya Mhe Zubeir mkoani Tanga ni sehemu ya matendo ya kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika uliofikiwa Aprili 26, 1964.
Amesema wapo baadhi ya watu wanaoibua ushawishi kwa wananchi wasijitokeze kushiriki uchaguzi huo, na kusema kwa kadri ya kasi ya maendeleo yaliyopo nchini, hoja hiyo inapaswa kuepukwa kwa vile haina tija.
Mhe Zubeir amesema, mfano mzuri wa umuhimu wa Serikali inayowajali wananchi kwa utumishi na utoaji huduma, ni mafanikio yanayoonekana kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Pia, Mhe Zubeir amegusia umuhimu wa kuulinda na kuuendeleza Muungano huo na kwamba katika miaka 61 ya uwepo wake, Watanzania wameshuhudia mambo mema mengi kuliko changamoto chache zinazojitokeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, pamoja na kumshukuru Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za miradi zilizotolewa mkoani humo, mafanikio ya ki-maendeleo yanadhihirika kwa pande zote za Muungano, hivyo ipo haja ya kuuendeleza na kuulinda.
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, wingi na thamani kubwa ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa Zanzibar na Tanzania Bara, vinadhihirisha umahiri wa uongozi na utawala wa Mhe Rais Dkt Samia na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Tanga, Mfaume Kizigo, amesema ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo, umechangia na ushirikiano uliopo kati ya Serikali, chama hicho na wakazi wa Tanga.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.