Na Mashaka Mgeta, HANDENI
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), Mhe Zubeir Ali Maulid, amesema miradi mikubwa inayotekelezwa kupitia sekta mbalimbali nchini, ni miongoni mwa ishara kuu za ubora wa uongozi wa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Mhe Maulid ameyasema hayo leo Aprili 24, 2025 baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi maabara ya Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Mji Handeni ambayo ni sehemu mradi uliogharimu Shilingi milioni 900.
Mhe Maulid yupo kwenye ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tanga, ikiwa ni katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa Aprili 26, 1964 na ‘kuizaa’Tanzania.
Amesema katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake, Mhe Rais Dkt Samia ametekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yakiwemo maboresho wa miundombinu na ujenzi wa maabara kwenye hospitali hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju amesema, mwaka 2023/2024, halmashauri hiyo ilipokea Shilingi milioni 900. Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 250 zilitumika kwa ujenzi wa maabara na Shilingi milioni 400 kwa ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU).
Pia, Shilingi milioni 111 zilitumika kwa ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti, Shilingi milioni 44,000,000 kwa ujenzi wa njia na Shilingi milioni 95 kwa ukarabati wa miundombinu chakavu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Mganga Mkuu wa Handeni Mji, Dk Hudi Shehdadi, ujenzi wa maabara hiyo uliofikia asilimia 81, ulianza Juni 14, 2024 na unatarajiwa kukamilika Mei 28, mwaka huu.
Amesema, maabara hiyo itahifadhi damu salama hivyo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto chini ya miaka mitano na kuongeza wigo na ufanisi katika kutoa huduma za kiuchunguzi wa magonjwa ya binadamu
Faida nyingine ni kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji vipimo vikubwa vya kimaabara kama vile uoteshaji wa vimelea vinavyosababisha usugu wa maradhi ya kuambukiza, ambao kwa sasa vinasafirishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga iliyopo umbali wa kilomita 160 kutoka Handeni.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.