Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
VIJANA 180 waliopata elimu kuhusu ushiriki wao kupata huduma za afya ya uzazi na kupiga vita vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, wametumia miaka mitatu kuwafikia wenzao 16,000 kupitia mfumo wa elimu rika katika kata 12 za wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Ujana Salama ‘unaoendeshwa’ na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Femina Hip, ukiwalenga vijana walio nje ya shule wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Femina Hip, Ruth Mlay amesema uenezaji wa elimu hiyo kupitia kwa vijana wenyewe, umechochewa na utayari wao na kwamba, takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2024, vijana takribani 10,000 walikuwa wameripoti kwenye vituo vya afya kupata huduma kama vile afya ya uzazi, utambuzi wa maradhi na upimaji afya.
Mlay aliyeongoza ujumbe wa Femina Hip, alifika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga jana Aprili 23, 2025 wakiwa katika ziara ya ufuatiliaji na tathmini ya mradi huo.
Pia amesema wanufaika hao wa mradi wa Ujana Salama wamepata ufahamu zaidi kuhusiana na masuala ya hedhi salama, namna ya kuepuka tabia hatarishi zinazosababisha mimba za utotoni na namna bora ya kudhibiti na kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na dhidi ya watoto.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Sebastian Masanja, aliipongeza Femina Hip kwa ufanisi uliopatikana kwenye mradi huo, na kushauri jitihada zaidi zifanyike kuzifikia wilaya nyingine za mkoa huo.
Masanja alisema, Serikali ipo tayari kuendeleza mahitaji muhimu kwa vijana kufikia malengo yao hususani yaliyoanishwa kupitia kwenye mradi huo.
Kuhusu kushamiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, Masanja amesema ipo haja kwa jamii kuwekeza zaidi katika malezi bora ya familia, ili kukijenga kizazi kinachotambua na kuthamini utu, upendo na uvumilivu.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.