Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imetenga na kutoa Shilingi milioni 100 kwa ajili ya uboreshaji wa soko kongwe la Ngamiani, ili kuweka mazingira yenye staha kwa wafanyabiashara na wateja wake.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Lusajo Gwakisa, amesema hayo alipotoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, aliyefanya ziara ya ghafla leo asubuhi, kufuatia kusambaa kwa picha mjongeo ikionyesha sehemu za soko hilo kuvuja maji yanayotokana na mvua zinazonyesha.
Gwakisa amesema uboreshaji wa soko hilo unatekelezwa na mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kazi hiyo, kampuni ya Ms Spacetec Corporatioon Limited.
Kwa mujibu wa Gwakisa, uboreshaji wa soko hilo ulioanza, ulisitishwa kutokana na ombi la wafanyabiashara waliotaka usitishwe ili wafanye biashara katika kipindi cha sikukuu za Idd el Fitr na Pasaka.
“Baada ta sikukuu hizo, zilianza kunyesha mvua zilizosababisha maeneo tuliyokusudia kuyaboresha, yakavujisha maji kama ilivyochukuliwa kwenye picha mjongeo iliyosambazwa kupitia mitandao ya kijamii,” amesema.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Ngamiani, Shaban Ramadhan aliyesema wanashirikiana na uongozi wa jijini la Tanga kukabiliana na changamoto zilizopo ikiwemo maeneo yanayovuja.
Ramadhan amesema picha mjongeo iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii, ‘imebeba’ ujumbe wa sauti wenye kupotosha kutokana na shutuma zinazotolewa kwa lengo la kuuaminisha umma kwamba hakuna jitihada zinazofanyika, jambo ambalo si kweli.
Mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo, Jonathan Mpanduka, amekemea hatua ya watu wasiokuwa na nia njema, kupiga na kusambaza picha zinazopotosha ukweli unahusu changamoto zilizopo kwenye soko la Ngamiani na namna Serikali inavyozitatua kwa kushirikiana nao (wafanyabiashara).
Kaimu Mhandisi wa Jiji la Tanga, Jumaa Jumanne, amesema miongoni mwa kazi zinazofanyika katika ukarabati wa soko hilo ni kuboresha mifereji yam aji machafu, kuondoa bati na ‘gata’ chakavu na kuweka mpya.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga kushirikiana na Mkandarasi huyo, kubuni namna bora ya kutekeleza ukarabati wa soko hilo pasipo kuwaondoa wafanyabiashara.
Pia, Mhe Dkt Batilda amesema, ukarabati huo unapaswa kufanyika kwa kasi ili ukamilike haraka, ikibidi kuongeza nguvu kazi zaidi ya inayotumika sasa.
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema mazingira bora kwa wafanyabiashara na watumiaji wa masoko ya bidhaa mbalimbali, ni miongoni mwa vipaumbele vya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, hivyo kuwahikikishia (wafanyabiashara wa Ngamiani) kwamba changamoto zinatatuliwa ndani ya muda mfupi.
Pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Mhe Balozi Dkt Batilda alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe Japhari Kubecha na Katibu Tawala Wilaya (DAS), Dalmia Mikaya.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.