Na Mashaka Mgeta, HANDENI
HAIKUWAHI kutokea kabla, kwa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kuwa na Chuo cha Uuguzi na Ukunga. Lakini Mei 2, 2025, historia imeandikwa, Chuo hicho kimejengwa, kimekamilika na kukabidhiwa rasmi kwa Serikali.
Chuo cha Uuguzi na Ukunga Kuwait, kimetokana na ushirikiano wa mashirika ya kiraia kutoka nchini Kuwait, Wakfu wa Al Noor Charity Association iliyofadhili mradi huo kupitia Islamic Help.
Mradi huo umehusisha majengo ya utawala, madarasa, maktaba, bweni, uzio, geti, samani na vitendea kazi, thamani ya jumla ni zaidi ya Shilingi bilioni 1.5, kwa mujibu wa Meneja Miradi wa Islamic Help, Abubakar Luchenya.
Akisoma taarifa kwa Waziri wa Afya, Mhe Jenister Mhagama, aliyekabidhiwa Chuo hicho kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe Dkt Philip Mpango, Luchenya amesema mradi huo utaendeleza mahusiano mema kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, na kuchagiza kasi ya uboreshaji wa sekta ya afya nchini.
Mwakilishi wa Balozi wa Kuwait nchini, Mussa Aldhubeid, amesema miongoni mwa matarajio kutoka kwenye Chuo hicho, ni kutimiza wajibu wa kuiwezesha jamii kuokoa, kukinga na kuponya magonjwa na visababishi vinavyoathiri afya za watu.
Mkurugenzi wa Al Noor Charity, Jamal Al Noor, amesema pamoja na msaada huo, taasisi yake inashughulikia maeneo yakiwemo mazingira, elimu na maji, miongoni mwa huduma nyingine zinazolenga kustawisha na kuboresha hali za wananchi.
Mwenyekiti wa Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Abdarahman Abdallah, amesema kukamilika kwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho, iliyotengewa ukurasa wa 131 hadi 143 kuelekeza uboreshaji wa sekta ya afya.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amesema azma ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuboresha afya za Watanzania, inajidhihirisha kupitia viashiria tofauti mkoani humo, ikiwemo utoaji wa Shilingi bilioni 72 kwa sekta ya afya katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake.
Ameitaja baadhi ya miradi na huduma zilizopatikana kupitia fedha hizo ni ujenzi wa zahanati 72, vituo vya afya 26, hospitali za wilaya sita (6) na ukarabati wa hospitali za tano.
Akihutubia hafla hiyo, Mhe Mhagama amewashuruku wafadhili na uongozi wa mkoa wa Tanga kwa kufanikisha mradi huo, na kuongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya upatikanaji na utoaji huduma bora za afya nchini.
Ametoa mfano wa ongezeko la wauguzi na wakunga wanaofikia 46,156 nchi nzima, na kwamba azma ni kuongeza idadi hiyo kadri ya mahitaji.
Pia Mhe Mhagama amesema Serikali inatilia mkazo kukuza utaalumu katika utoaji tiba lishe ili kuiwezesha jamii kukabiliana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.