MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian (pichani) leo saa moja asubuhi, amepiga kura katika kituo cha Raskazone Swimming Club, akiwa miongoni mwa maelfu ya wakazi wanaoendelea kushiriki zoezi hilo kwenye maeneo tofauti mkoani humu.
Mhe Balozi Dkt. Batilda, amewahimiza wakazi wa Tanga kujitokeza kwa wingi zaidi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu huu wenye ishara za amani na utulivu, huku akielezea kufurahishwa na hali ya hewa, maandalizi na mwitikio wa wapiga kura vituoni.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutupa hali nzuri ya hewa leo. Wote wenye sifa tujitokeze, tupige kura kwa amani na bila hofu,” amesema Mhe Balozi Dkt. Batilda.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Almachius Mchunguzi, amesema Tanga bado ipo shwari kwenye maeneo yake yakiwemo ambayo wananchi wanayatumia kupigia kura.
Akizungumza na waandishi baada ya kupiga kura kituoni hapo, ACP Mchunguzi ametoa rai kwa wapiga wenye sifa kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kutimiza haki ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaofaa.
Hata hivyo, ACP Mchunguzi amesema vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo vinaendelea kutekeleza majukumu yake yakiwemo ya kiintelijinsia, ili kubaini na kudhibiti vitendo vyovyote vitakavyoashiria uvunjifu wa amani ama kutaka kuathiri mwenendo wa upigaji kura.
”Hali kwa ujumla ipo shwari na wananchi wenye sifa ya kupiga kura wasisite kujitokeza kwa wingi kwenda kuwachagua viongozi wao,” amesema.
Upigaji kura unaendelea ukitarajiwa kuwashirikisha wapiga 1,632,737 wenye sifa za kuwachagua Rais, Wabunge na Madiwani kwenye vituo 4,527 vilivyopo mkoani Tanga.
MWISHO
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.