Na Mashaka Mgeta, MOROGORO
MAAFISA Mawasiliano wa Serikali (GCUs), wametakiwa kuchagiza azma ya kuleta tabasamu kwa Watanzania, kupitia utoaji taarifa sahihi na ushirikishaji vyombo vya habari kutangaza mafanikio kutoka kwenye miradi ya maendeleo na huduma za jamii.
Wakuu wa GCUs na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wameyasema hayo kwenye Mafunzo ya Faida ya Matumizi ya Miundombinu na Mifumo ya Tehama ya Serikali kwa Wananchi yanayofanyika mjini Morogoro.
Akilizindua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alisema,”...mwisho wa utumishi wa awamu ya sita, usipimwe tu kwa vitu vitakavyoachwa, bali pia kwa tabasamu la utu litakaloachwa kwenye nyuso za Watanzania..:
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA katika TAMISEMI, Erick Kitali, amesema, wakati Mhe Rais Dkt Samia akilenga kuleta tabasamu kwa Watanzania, ni wajibu wa Maafisa Mawasiliano, Habari na Mahusiano Serikalini kufanikisha azma hiyo kupitia utekelezaji wa majukumu ya siku kwa siku.
Kitali amesema, tabsamu la Watanzania linategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano, ili wananchi waijue miradi na huduma za maendeleo na ustawi wao, na namna ya kunufaika nazo.
Amesema, miongoni mwa taarifa hizo zinazohusu matumizi ya mifumo ya mawasiliano ya Serikali inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati na pasipo kutumia gharama kubwa.
Kwa mujibu wa Kitali, wananchi wanapaswa kujulishwa umuhimu wa minara ya mawasiliano iliyojengwa kwenye maeneo tofauti nchini, kwamba inafaa kwa kupata huduma kupitia mifumo hiyo, badala ya uelewa wa matumizi ya simu za kiganjani pekee.
Naye Mkuu wa GCU na Msemaji wa TAMISEMI, John Mapelele, amesema dhana ya ’Watanzania wenye tabasamu’, pamoja na mambo mengine, inategemea upatikanaji wa taarifa sahihi za maendeleo na huduma bora zinazopatikana nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya TEHAMA wa TAMISEMI, Melkiori Baltazari, amehimiza ushirikiano kati ya GCUs na TEHAMA kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha mnyororo wa uchakataji na utoaji taarifa kwa wakati na usahihi.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.