Na Mashaka Mgeta, PANGANI
WADAU wa shughuli za maendeleo, biashara na uchumi mkoani Tanga, wameaswa kulipa kodi kwa uadilifu na uaminifu, ili kuongeza mapato ya ndani yatakayoziwezesha halmashauri za jiji, miji na wilaya kutoa kiasi kikubwa zaidi cha mikopo kwa vijana inayotokana na mapato ya ndani kwa vijana.
Mikopo hiyo inayotolewa kila baada ya miezi minne, inatokana na asilimia 10 ya mapato hayo, na kuelekezwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mgawanyo wa mikopo hiyo unatolewa kwa uwiano wa asilimia nne kwa vijana, asilimia nne kwa wanawake na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe Ayubu Sebabili ameyasema hayo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, kusikiliza kero za wananchi na kutangaza fursa za kiuchumi kwa vijana mkoani humo.
Mhe Sebabili, alikuwa akijibu hoja ya mmoja wa vijana walioshiriki kikao hicho, Omar Kidau, ambaye pamoja na kushukuru kikundi chake cha Hatupoi Boda Group kupata mkopo ulioanzia Shilingi milioni 6 na sasa kufikia Shilingi milioni 27.6, baadhi ya vikundi havijanufaika.
Akatoa mfano kuwa kikundi chake kilikuwa miongoni mwa vikundi 26 vilivyopata mikopo kati ya 69 vilivyoomba.
Mhe Sebabili akasema, kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, uchache wa mapato ni chanzo cha kuwepo ukomo mdogo wa mikopo hiyo.
Kwa upande mwingine, vijana wa Pangani, wakaiomba Serikali kuitenga wilaya hiyo dhidi ya kufungia shughuli za kiuchumi, zinapotokea vurugu kama maandano yasiyoruhusiwa kwenye maeneo mengine ya nchi.
Amani Rashid, kwa niaba ya vijana wengine, akasema wanatambua umuhimu wa amani na utulivu, hivyo haiwezi kutokea kwa vijana wa Pangani kuandamana ama kufanya vurugu.
”Yakitokea maandamano ama vurugu, huku Pangani hakuna wa kuingia barabarani ama kufanya vurugu, hivyo kama ni kufungia shughuli za biashara tunaomba Pangani isiwe miongoni mwa maeneo ya kufungiwa,” amesema.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.