Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza wakazi wa mkoani Tanga, kutumia fursa ya ukosefu wa maduka ya kubadili fedha za kigeni, kusajili na kupata leseni za biashara hiyo yenye tija kwa uchumi wa Taifa, maendeleo na ustawi wao.
Rai hiyo imetolewa na wataalamu wa BoT, waliokutana na wafanyabiashara wa shughuli zinazohusiana na sekta ya fedha mkoani humo, katika kikao kilichofanyika leo Mei 9, 2025 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mkaguzi Mwandamizi wa BoT, Jaribu Walii, amesema Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassa, imesikiliza hoja za wadau wa sekta ya fedha na kuweka mazingira rafiki kwao, wakiwemo wafanyabiashara wa sekta hiyo kuanzisha maduka ya kubadili fedha za kigeni.
Miongoni mwa mazingira hayo ni maboresho ya Kanuni za Biashara ya Fedha za Kigeni yaliyowezesha kushusha mtaji wa uwekezaji kwa leseni za daraja B kutoka Shilingi bilioni 1 hadi Shilingi milioni 200, na wamiliki wa hoteli zenye kuanzia hadhi ya nyota tatu, kutohitaji kiasi cha mtaji wa ziada zaidi ya uwekezaji walioufanya kwenye hoteli.
Meneja Usimamizi Taasisi Maalum za Fedha wa BoT, Suzan Katabi, amesema ukaguzi wa hivi karibuni mkoani Tanga, ulibaini kuwepo wafanyabiashara kadhaa wanaojihusisha na kubadili fedha pasipokuwa na leseni, hali inayowaweka katika hatari ya makosa jinai ‘yanayoangukia’ kwenye uhujumu uchumi.
Katabi, amesema kuna madhara makubwa kwa muuzaji na mnunuzi wa fedha za kigeni kupitia ‘soko haramu’ ikiwemo uvunjifu wa sheria, upotevu wa mapato na ukosefu wa takwimu za uhalisia wa biashara ya kubadilisha fedha nchini.
Wafanyabiashara waliochangia kwenye mkutano huo, wamesema zipo changamoto kadhaa zinazoikabili biashara ya kubadilisha fedha ikiwemo ukosefu wa maduka, hivyo kutegemea mabenki ambayo hayabadilishi fedha za nchi jirani hususani Kenya na Uganda ambazo wasafiri (wateja) wengi wanakwenda ama kutoka huko.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.