Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
KESHO, Febrauri 13, mwaka huu inatarajiwa kuwa yenye shangwe, nderemo na vifijo kwa wakazi wa Tanga, watakapokusanyika kwenye kijiji cha Mkata wilayani Handeni, kumpokea Waziri Mkuu, Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba.
Mhe Dkt. Mwigulu, atafanya ziara ya siku tano, kuanzia Februari 13 hadi 17, 2026, akizitembelea halmashauri 11 zilizopo kwenye wilaya nane za mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake leo kuwa ziara hiyo ya kwanza ya Mhe Dkt. Mwigulu, tangu ateuliwa Novemba 13 na kuapishwa kwa wadhifa huo Novemba 14, 2025, itakuwa ya pekee, ikionesha mahaba ya wakazi wa Tanga kwa kiongozi huyo na Serikali ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, atakapowasili, Mhe Dkt. Mwigulu atasalimiana na wananchi, kisha kutembelea Kituo cha Kupoozea Umeme kilichopo Mkata, na kupata taarifa ya ujenzi wake.
Amesema, akapotoka hapo, Mhe Dkt Mwigulu, atakwenda Halmashauri ya Mji Handeni kukagua na kufungua jengo la Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na siku inayofuata, atatembelea mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi ambapo atakagua na kuweka jiwe la msingi, kisha kuzungumza na wananchi.
“Baada ya hapo, atatembelea mradi wa maji Kwamaligwa na kupata taarifa ya maji, kukagua tenki la maji kisha kusalimiana na wananchi,” amesema.
Mhe Balozi Dkt. Batilda amesema, baada ya mradi huo wa maji, atakwenda wilayani Korogwe ambapo atapata taarifa na kukagua mradi wa maji wa miji 28 utakazinufaisha jamii za wilaya hiyo, Pangani, Muheza na Handeni.
Kwa mujibu wa Mhe Balozi Dkt Batilda, Februari 15, 2026, Mhe WDkt. Mwigulu, atakwenda Wilaya ya Mkinga kukagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa tawi la Chuo Kikuu cha Mzumbe na kusalimiana na wananchi.
“Baada ya hapo, Mhe Waziri Mkuu Mwigulu atatembelea bandari ya Tanga, atakapopokea taarifa, kukagua na kuzungumza na wafanyakazi wa bandari na jioni yake atahutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Lamore jijini Tanga.
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, Februari 16, 2026, Mhe Dkt Mwigulu atakagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, kisha kuzungumza na wananchi.
Akimaliza kuzungumza na wananchi, Mhe Mwigulu atatembelea kiwanda cha Yogi Polypack uzalishaji wa vifungashio, Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) eneo la Chongoleani na daraja la Mto Pangani kisha kusalimiana na wananchi wa Pangani.
Amesema, akitoka Pangani, Mhe Dkt. Mwigulu atakwenda wilayani Lushoto atakapopata taarifa, kukagua na kuifungua hoteli ya Java na Februari 17, 2026, atatembelea Hospitali ya Wilaya kukagua mradi wa jengo la Oksijeni, kukagua, kulizindua, kisha kusalimia wananchi.
Pia, siku hiyo, Mhe Dkt. Mwigulu atatembelea, kupata taarifa, kukagua na kuzindua Shule ya Amali Majulai iliyopo kata ya Mlalo, kisha kusalimia wananchi.
”Akimaliza kuzindua shule hiyo ambayo ni mpya, msafara wa Mhe Waziri Mkuu Mwigulu utakwenda Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kwa ajili ya kikao cha majumuisho na baadaye kuondoka kuelekea mkoani Kilimanjaro,” amesema Mhe Balozi Dkt Batilda.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.