COPRA YAGAWA TANI 1.35 YA MBEGU ZA UFUTA TANGA
Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imegawa tani 1.35 (sawa na kilo 1,350) kwa wakulima wa halmashauri tatu kati ya 11 za mkoani Tanga.
Mbegu hizo zimetolewa jana Januari 29, 2026 ambapo Afisa Kilimo COPRA wa Kanda ya Kaskazini, Paskalia Sitembela, alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe Ayubu Sebabili, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian.
Sitembela alisema gharama za ununuzi wa mbegu hizo zilizosambazwa kwenye halmashauri za wilaya ya Handeni, Pangani na Mji Handeni, ni sehemu ya tozo ya iliyopatikana kwenye mauzo ya tani 7 za mazao kwa njia ya stakabadhi ghalani msimu uliopita, na kupatikana takribani Shilingi bilioni 9.
Naye Mhe Sebabile amesema, mbegu hizo zitaleta tija na uzalishaji mkubwa wa mazao bora yanayokidhi matakwa ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) inayoeleza; “kutokomeza njaa, kufanikisha usalama wa chakula na lishe iliyoboreshwa.”
Aidha, sehemu ya sekta za kimageuzi katika Dira hiyo inaeleza kuwa, kilimo ni sekta ya kisasa, yenye tija, na ustahimilivu kwa kutumia teknolojia za kisasa, kuongeza uzalishaji na thamani za mazao na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika.
Pia Dira ‘inatamka’ kwamba Tanzania itakuwa ghala la chakula linaloaminika Afrika, na kinara wa kimataifa katika mazao muhimu kama korosho, kahawa, mbogamboga, huku ikiboresha uzalishaji endelevu katika mifugo, uvuvi na mifugo.
Mhe Sebabile amewawahiza wakulima mkoani humo, kuongeza tija kwenye kilimo cha mazao mchanganyiko ili kuleta ufanisi kupitia fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.
Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Mkoa wa Tanga, Mhandisi Emigius Kasunzu, amesema Serikali imefanikiwa kupata suluhu ya changamoto mbalimbali zilizoikabili sekta ya kilimo.
Miongoni mwake ni utoroshaji wa mazao uliodhibitiwa kwa kuweka vituo vya ukaguzi barabarani na uuzaji ama uvunaji wa mazao kabla ya kukomaa ambapo wakulima wameelimishwa kuhusu madhara yake na kuacha kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kasunzu, matumizi ya mbegu zilizokosa ubora ilikuwa miongoni mwa changamoto inayoondoka kupitia matumizi ya mbegu bora zikiwemo zilizotolewa jana.
Meneja Mkuu wa TARECU (2025) Limited, Rashid Mziray, amesema ongezeko la mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kutoka korosho pekee, ni miongoni mafanikio na ishara za ukuaji wa kilimo mkoani Tanga.
Amesema, ongezeko la mazao mchanganyiko lilianza msimu wa 2024/25 kupitia COPRA, na kutumika kwenye halmashauri za wilaya ya Handeni, Pangani, Mji Handeni, Kilindi na Muheza.
Naye Mkulima Waziri Athumani kutoka Pangani, akizungumza kwa niaba ya wenzake, amesema matumizi ya mbegu bora zilizotolewa, yatakuwa chachu kwa watu wengi kushiriki zaidi kilimo kutokana na tija inayopatikana.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.