Na Mashaka Mgeta, PANGANI
KATIBU Tawala Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, amewaongoza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi mkoani humo katika ziara ya utalii wa ndani kwenye Hifadhi ya Taifa Sadaani.
Ziara hiyo ilifanyika jana baada ya kikao cha Baraza hilo kilichojadili masuala mbalimbali ya utendaji kazi na utoaji huduma.
Nyuso za walio wengi miongoni mwa wajumbe amba oni watumishi katika Sekretarieti ya Mkoa, zikaonekana zenye furaha na bashasha, walipoianza asubuhi ya Januari 28, 2026 kwa kutembelea maeneo tofauti ya Hifadhi ya Taifa Saadani.
Mchatta anasema hatua ya kufanya kikao cha Baraza hilo kwenye hifadhi hiyo, kisha ‘kuunganisha’ na utalii wa ndani, ni sehemu ya uendelezaji wa mazingira bora ya kazi na uboreshaji wa fikra na akili, vitumike vema kutafsiri na kufanya uamuzi sahihi kwa utendaji kazi na utoaji huduma kwa jamii.
Safari iliyoanzia kwenye maeneo tofauti ya makazi ya watalii hifadhini, iliwafikisha watumishi hao ‘huku na kule’ na kuwaona wanyama wa aina na tabia tofauti.
Miongoni mwa Waongoza Watalii, Hamis Shaban, akataja aina tofauti za utalii uliopo Saadani ikiwemo wa kutembea kwa miguu, kutazama Wanyama wanapokusanyika ufukweni mwa Bahari wakati wa usiku kutokana na kuvutiwa na harufu ya maji, na kusafiri kwa ngalawa kwenye mto Wami wenye mamba na viboko ‘wa kutosha’.
Watumishi hao wakiongozwa na Mchatta, wakasafiri kwa ngalawa kwenye Mto Wami na kufika maeneo kama vile yenye mazalia ya viumbe wa majini na kwenye mlango bahari, unapounganika mto huo na Bahari ya Hindi.
Shaban anasema kwenye mlango Bahari huo, maji baridi kutoka Mto Wami yanachanganyika na maji chumvi ya baharini, hivyo kuifanya ekolojia ya eneo hilo kuwa moja ya vivutio bora vya utalii.
Pia, Shaban anaelezea tabia za Wanyamapori wakiwemo wanaokula na wanaoliwa na wanyama wengine.
Mmoja wa watumishi hao, Lucy Jacob, anasema ziara hiyo ‘imewafumbua macho’ zaidi kwa kuwafikisha eneo la mapumziko, wanalopaswa kulitumia hata wanapokuwa na familia, ndugu, jamaa na marafiki.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.