Na Mashaka Mgeta, PANGANI
ZIARA ya utalii wa ndani iliyofanywa na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa (RS), ikiongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, kwenye Hifadhi ya Taifa Saadani, inaweza kuonekana tukio la kawaida.
Lakini kwa uongozi wa hifadhi hiyo, ziara hiyo ya Januari 28, 2026, imebeba ujumbe mzito kwa taasisi za umma na binafsi, kufanya vikao vyake huko Saadani.
Mkuu wa Hifadhi ya Saadani, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Gladys Ng'umbi, anaitaja ziara hiyo ya kwanza inayohusisha kufanya vikao na utalii hifadhini humo, kwamba ‘imefungua milango’ na kuthibitisha kwamba mahali hapo panafaa zaidi kwa vikao.
Ng’umbi anasema RS ya Tanga haikubahatisha kufanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwenye hifadhi hiyo, kwani mazingira yake ni tulivu na pembezoni mwa Bahari ya Hindi kuna hewa nzuri inayopenya kupitia kwenye miti ya mikoko.
“Mmefanya jambo kubwa sana katika sekta ya utalii hasa kuwa mfano kwa taasisi nyingine za umma na binafsi kuja kufanya vikao vyao hapa,” anasema muda mfupi, kabla ya kuagana na ujumbe wa RS Tanga.
Gladys anataja baadhi ya sifa za hifadhi hiyo, pamoja na Wanyama, kuna ekolojia ya maji chumvi ya baharini kuchanganyika na maji baridi ya Mto Wami, hivyo kuvifanya viumbe kama samaki kuishi kwenye mazingira hayo, jambo lisilokuwa la kawaida.
Ndani ya Mto Wami kunapofanyika utalii wa usafiri wa ngarawa, Gladys anasema wamo viboko wanaoishi kwenye maji baridi yaliyochanganyika na maji chumvi, na wanapotoka nje kuota jua, ngozi yao inakuwa nyekundu na kuvutia zaidi kuwatazama.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.