Na Mashaka Mgeta, LUSHOTO
WATANZANIA wametakiwa kutumia miundombinu bora inayojengwa na kuboreshwa kwenye maeneo tofauti ya kisekta, iwanufaishe kupitia fursa mbalimbali, yakiwemo masoko ya bidhaa zao nje ya nchi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Dk Ashatu Kijaji ameyasema hayo jana Januari 8,2025, wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mnada wa awali uliopo katika kijiji cha Kisima, kata ya Lunguza wilayani Lushoto, mkoa wa Tanga.
Mradi huo uliofikia asilimia 90 na kugharimu Shilingi 399,175,753.40, kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, George Medeye, utakuza biashara hususani ya mifugo na mazao yake kwa masoko ya ndani nan je ya nchi.
Mhe Dk Kijaji amesema, ubora wa miundombinu iliyopo kwenye maeneo tofauti ya kisekta ikiwemo mnada huo, ni miongoni mwa nyenzo zilizowekezwa na Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kukuza uchumi, maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake.
Kwa mujibu wa Mhe Dk Kijaji, hatua za awali katika utawala wake, Mhe Rais Dk Samia alifungua mipaka zaidi kikanda na kimataifa, hali inayowavutia wawekezaji na wafanyabiashara wengi kuja nchini, kuchochea ongezeko la uzalishaji na bei za bidhaa za ndani.
‘’Ni kwa sababu hiyo, mnada huu unakwenda kuongeza ubora na usalama wa biashara ya mifugo hadi kwenye masoko ya nje ya nchi, na bei ya mifugo itaongezeka,’’ amesema.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Medeye, amesema ili kukamilika na kufanya kazi kwa ufanisi, mnada huo unahitaji ongezeko la fedha ili kukamilisha miundombinu ya ofisi, mizani, mabanda na za kushusha na kupakia mifugo.
Diwani wa Kata ya Lunguza, Mhe Yassin Bila amesema ingawa hajawafikia, lakini wingi wa miradi inayotekelezwa na Serikali ni kielelezo cha uwepo wa Mhe Rais Samia kwenye maisha yao na jamii nyingine zinazoishi pembezoni mwa mikoa.
Leo Mhe Dk Kijaji anaendelea na ziara yake katika wilaya ya Korogwe na kesho atakuwa Handeni kabla ya kuhitimisha ziara hiyo Kilindi
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.