Kongamano la kihistoria la Uwekezaji lafana Tanga
Na Emma Kigombe, TANGA
KONGAMANO la Kutangaza na Kuzindua Mwongozo wa Fursa za Uwekezaji, Biashara na Utalii mkoani Tanga, limefanyika kwa ufanisi mkubwa likiwashirikisha wadau kutoka sehemu tofauti za ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, akiwakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji na Mipango), Profesa Kitila Mkumbo, alifungua kongamano hilo lililofanyika Novemba 16 na 17, 2023 jijini Tanga, na kuzindua Mwongozo wenye kuainisha fursa za uwekezaji, biashara na utalii zilizopo mkoani Tanga.
Miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo la pili mkoani Tanga, baada ya jingine lililofanyika miaka 10 iliyopita walikuwa wawekezaji wa ndani na wale wa nje walioshiriki kwa njia ya mtandao na mabalozi wa Tanzania waliopo nchi tofauti duniani walioshiriki pia kwa njia ya mtandao.
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, waliowahi kuwa Wakuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigila (ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Geita) na Adam Malima (Mkuu wa Mkoa wa Morogoro), Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Profesa Mkumbo akasema Mwongozo uliozinduliwa utahamasisha zaidi uwekezaji wa ki-mkakati utakaochochea maendeleo ya uchumi na kuweka msisitizo katika uwekezaji endelevu unaowajibika kwa mazingira na manufaa kwa jamii.
Profesa Mkumbo amesema, Mwongozo huo umeeleza kwa kina fursa za kiuchumi zinazopatikana mkoani Tanga na ambazo zinaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika masuala ya biashara na uwekezaji, lengo likiwa ni ‘kuifungua nchi’ kwa kuwakaribisha wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali ya kisekta nchini.
”Falsafa inayomwongoza Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassani katika masuala ya biashara na uwekezaji ni kufungua nchi, fedha hazitengenezwi na Serikali bali zinatengenezwa na wawekezaji,’’ amesema na kuongeza…
‘’Kwa hiyo kazi ya Serikali tuliyoahidi ni kuweka mazingira rafiki na mazuri ili watu wafanye biashara itakayotengeneza ajira na watu wapate kipato kupitia ajira hizo.”
Profesa Mkumbo amesema umuhimu wa sekta binafsi unatokana na mchango wake mkubwa katika kutengeneza ajira ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kati ya ajira 95 kati ya 100 zilizopo nchini, zinatengenezwa na sekata binafsi wakati tano pekee zinatoka serikalini na taasisi za umma.
Profesa Mkumbo akaelekeza mamlaka zinazohusika kwenye mchakato wa uwekezaji nchini, kuondoa urasimu usio wa lazima kiasi cha kuwakatisha tamaa wawekezaji wenye nia thabiti ya kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Kwa hali hiyo, Profesa Mkumbo akaziagiza mamlaka za serikali za mitaa kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji na kuyawekea miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji na umeme.
Kwa upande wa fursa za uchumi wa buluu, Profesa Mkumbo ameutaka mkoa wa Tanga usimamie suala la uvunaji endelevu wa mazao ya bahari ili kila raia aweze kunufaika na rasilimali hiyo
“Tanga ina kila aina ya samaki, jielekezeni kufanya uvuvi endelevu na kuongeza thamani ya mazao ya bahari ili kila mmoja anufaike na uwepo wa bahari na mazao yake,” amesema Profesa Mkumbo.
Mwisho
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.