MAJALIWA AWATAKA TANGA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI
Na Mashaka Mgeta, TANGA
WAZIRI Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa amewahimiza wakazi wa mkoa wa Tanga, kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazofunguka na kuunganisha mkoa huo na maeneo mengine ya ndani na nje ya nchi.
Mhe Majaliwa amesema hayo leo wakati akizungumza kwenye eneo la Kange mjini hapa, baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la kitega uchumi la Dk Samia Suluhu Hassan Business Centre, lililogharimu takribani Shilingi bilioni 8.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo bandari wa Tanga, ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadan – Bagamoyo, uchumi wa bluu vimezidi kuboreshwa, hivyo kuwataka wakazi hao kufanya kazi halali ili kuwa miongoni mwa wanufaika wa fursa hizo.
‘’Kila mtu afanye kazi kwenye sekta yake ya uzalishaji, kwa maana kutokana na uwepo wa rasilimali nyingi, ubora wa miundombinu na viongozi wazuri wanaoletwa hapa mkoani kwenu, Tanga sasa haina sababu ya kutosimama kiuchumi,’’ amesema.
KUREJESHA HESHIMA YA VIWANDA
Mhe Majaliwa amesema, Serikali inaendeleza mpango wa kufufua viwanda vikiwemo vya mkoani Tanga ambapo kuna kiwanda cha saruji kinachotarajiwa kuwa kikubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kuhusu uchumu wa bluu, Mhe Majaliwa amehimiza uwekezaji zaidi katika sekta hiyo, kutokana na tafiti kadhaa kuonyesha kupungua kwa idadi ya walaji wa samaki nchini kunakotokana na uchache wa wavuvi.
Katika kuchangia jitihada za kukuza uvuvi, Mhe Majaliwa amesema Rais Dk Samia amenunua boti za kisasa za uvuvi 222 zinazogawiwa nchi nzima, huku kukiwa pia na uingizaji wa teknolijia ya kufuga samaki kwenye vizimba baharini na kwenye maziwa.
Kwa mujibu wa Mhe Majaliwa, majaribio ya ufugaji samaki yanafanyika kupitia vizimba 500 vilivyopo kwenye maziwa ya Tanganyika na Viktoria.
AWAASA WAFANYABIASHARA KUITUMIA BANDARI YA TANGA
Mhe Majaliwa amewahimiza wafanyabiashara nchini kuitumia bandari ya Tanga iliyoboreshwa kwa mradi uliogharimu Shilingi bilioni 256.5, ili kuepukana na msongano kwenye bandari nyingine zilizo nje ya Tanga.
Amesema uboreshaji wa bandari hiyo umeiongezea uwezo wa kuhudumia shehena kutoka 750,000 kufikia 300,000.
Akizungumzia ujenzi wa uwanja wa ndege mkoani humo, Mhe Majaliwa amesema zabuni ya ujenzi wake imeshatangazwa, kwa vile Tanga na Lindi ilibaki kuwa mikoa pekee ambayo viwanja vyake havijajengwa.
Amesema nia ya Mhe Rais Samia ni kuona ndege zote 14 za Shirika la Ndege Tanzania (ATC) zinawahudumia wananchi na kutua kwenye mikoa yote nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amesema jengo la kitega uchumi cha Dk Samia Suluhu Hassan Business Centre ni miongoni mwa miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.6 zilizotolewa na Rais Dk Samia.
Mhe Balozi Dk Burian amesema miongoni mwa miradi iliyonufaika kupitia fedha hizo ni ujenzi wa shule mpya 27 uliogharimu Shilingi bilioni 159, ongezeko la hospitali za wilaya kutoka mbili hadi sita uliogharimu Shilingi bilioni 36, upatikanaji umeme kwenye vijiji 749 kati ya 779 vya mkoani humo na miradi kadhaa ya maji iliyogharimu Shilingi trilioni 1.2.
Amesema hivi sasa, mkoa huo unaendelea kuwahimiza wananchi ‘kuzichangamkia’ fursa za uwekezaji zikiwemo zilizoainishwa na Mhe Majaliwa.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.