Na Mashaka Mgeta, ZANZIBAR
KAMISAA wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mhe Anne Makinda, amesema Maafisa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali wanapaswa kuisemea Serikali kwenye maeneo yao, ikiwa ni sehemu ya kusaidia utendaji kazi wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Mhe Makinda ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye Kikao Kazi cha Maafisa hao katika ngazi za wizara, mikoa na halmashauri, kilichofanyika Unguja, Zanzibar kati ya Aprili 3-6, mwaka huu.
Amesema katika kuisemea Serikali kupitia vyombo vya habari vya taasisi zao, na ushirikishaji Waandishi wa Habari, Maafisa hao wanapaswa kuwekeza zaidi kwenye matumizi ya takwimu sahihi.
Kwa mujibu wa Mhe Makinda, hatua hiyo itatoa picha yenye kuakisi uhalisia wa mafanikio ya utendaji kazi wa Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
“Msimuache Msigwa peke yake (Msemaji Mkuu wa Serikali) kuisemea Serikali, na ninyi Maafisa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Itifaki mna jukumu hilo kwenye maeneo yenu,” amesema.
Mhe Makinda aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali kama vile ubunge, uwaziri na Spika, amesema Maafisa hao wanahusika na tasnia ya habari yenye umuhimu mkubwa katika ushirikiano wenye lengo la kuijenga nchi, hivyo kusisitiza msingi wa matumizi ya takwimu kwenye kazi zao.
Akiwasilisha mada kuhusu ‘Matumizi ya Takwimu kwa Maendeleo Endelevu,” Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt Msengwa, akasema takwimu sahihi zinapotumika kwenye taarifa na habari, zinasaidia katika kuhoji, kujiridhisha na kuepusha ukinzani na kwamba ni muhimu zikatafsiriwa ipasavyo kabla ya kuzifikisha kwa ‘walaji’.
Amesema ni jambo ‘linaloimiza jamii’ na NBS ikiwemo, zinapotolewa taarifa ama habari potofu, licha ya kuwepo takwimu sahihi zilizochakatwa na kuridhiwa kwa matumizi ya kuwafikia wananchi.
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Grison Msigwa akasema uhakika wa habari na taarifa, unapata nguvu zaidi kupitia matumizi ya takwimu sahihi yanayopaswa kuwa sehemu muhimu kwa Maafisa hao na Waandishi wa Habari nchini.
Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyeshiriki na kuongoza Kikao Kazi hicho kwa takwibani nne, akawaasa Maafisa hao na Waandishi wa Habari, kujikita katika kuandika masuala badala ya matukio pekee.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.