Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
KASI ya kuunganisha mifumo wa mawasiliano kwenye mkongo wa taifa wa mawasiliano, inakidhi malengo ya Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kuchochea maendeleo na ushirikiano kwa nchi za mashariki na kusini mwa Afrika.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Jerry Silaa, ameyasema hayo alipozungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Brian ofisini kwake jijini Tanga, leo Januari 23, 2025.
Mhe Silaa yupo mkoani Tanga kwa ziara ya siku moja, kukagua mkongo wa taifa wa mawasiliano kwenye eneo la Horohoro kwenda Kenya, kupitia Mombasa.
Amesema mabadiliko ya mifumo wa kijamii, maendeleo na uchumi, yametoa mwanya wa matumizi makubwa ya teknolojia ya mawasiliano, hivyo kuchangia umuhimu wa mkongo wa taifa kwa maendeleo na mahusiano ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani.
Mhe Silaa amesema, kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Mhe Rais Dk Samia, imefanikisha kuziunganisha wilaya 106 kwenye mkongo huo na kwamba jitihada za kumalizia wilaya 30 zilizobaki zinaendelea.
Naye Mhe Balozi Dk Batilda, amesema ufanisi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano unaoziunganisha Tanzania na Kenya (kutokea Mombasa) utainufaisha Tanga katika nyanja mbalimbali za kijamii.
Mhe Balozi Dk Batilda amesema kupitia maboresho na ujenzi wa miundombinu ikiwemo bandari, uwanja wa ndege na barabara, umuhimu wa sekta ya mawasiliano unazidi kukua kwa maendeleo na ustawi wa wakazi wa mkoa huo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.