Na Emma Kigombe, OMM TANGA
KATIBU Tawala wa Mkoa (RAS) wa Tanga, Rashid Mchatta, amehitimisha mafunzo ya utekelezaji wa Mwongozo wa Kupima Uwajibikaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia mfumo wa kidijitali wa iMES, akiutaja kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha utendaji wa halmashauri katika kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho kilichofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 19 Agosti 2025, Mchatta amesema Tanga imeonesha mafanikio ya awali ambapo kiwango cha uwajibikaji katika halmashauri 11 za mkoa huo, kimefikia zaidi ya asilimia 60 kwa mwaka 2024/25, kupitia mfumo huo unaosimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
“Huu ni ushahidi wa wazi kuwa jitihada zetu zinaanza kuzaa matunda. Hata hivyo, bado tunalo jukumu kubwa la kuimarisha zaidi uwajibikaji kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Serikali,” amesema.
Mchatta ameishukuru TAMISEMI, Taasisi ya WAJIBU inayoongozwa na FCPA Ludovick Utouh na Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) kwa mchango mkubwa katika maandalizi na usimamizi wa mwongozo huo.
Amesema, iMES itatumika kufanya upimaji wa utendaji katika kila robo mwaka, ambapo kutakuwa na upimaji wa ndani na wa nje ili kuhakikisha taarifa zinazoandikwa zinathibitishwa na kutoa matokeo halisi ya utendaji kwa kila halmashauri.
Mchatta amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mwongozo huo, ili kuhakikisha maeneo yote yaliyoainishwa yanafanyiwa kazi kikamilifu.Katika hatua nyingine, alikumbusha watumishi wa umma kujiepusha na lugha za kisiasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, na badala yake wajikite katika kutimiza wajibu wao wa kikatiba kwa kuwahudumia wananchi, na kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi huo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.