SILAA: TUMIENI TAASISI BINAFSI KUPIMA ARDHI, KUPANGA MIJI
Na Mashaka Mgeta, OMM – TANGA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe Jerry Silaa, ameelekeza kutumia taasisi za binafsi kusaidia mipango ya kupima ardhi na kupanga miji nchini ili kupata ufanisi kwa haraka.
Mhe Silaa ameyasema hayo jana, Aprili 23, 2023 wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa kliniki ya ardhi iliyoanza mkoani hapa Aprili 22 na kufikia kilele chake Aprili 28, 2024.
Mhe Silaa amesema upimaji ardhi na upangaji miji ni sehemu ya mahitaji muhimu yanayochangia utatuzi wa migogoro inayohusiana na sekta hiyo, na kuwapata wamiliki fursa pana zaidi kiuchumi.
Amewataka wataalamu wa ardhi wakiwemo Wapima Ardhi, Maafisa Mipango Miji na Maafisa Ardhi kutekeleza wajibu ipasavyo, ili kudhibiti vitendo vinavyofanywa na watu wasiotambulika kisheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Hata hivyo, Mhe Silaa amewataka wananchi wakiwemo wa mkoani Tanga, kujiepusha wa utekelezaji wa majukumu yasiyowahusu kuhusiana na masuala ya ardhi ikiwemo uwekaji wa mipaka, upangaji matumizi na umilikishaji wa ardhi.
Amesema kazi hizo zina wataalamu wake ambao ni Wapima Ardhi, Maafisa Mipango Miji na Maafisa Ardhi waliopo nchi nzima.
ASISITIZA SIKU MBILI KWA WATAALAMU WA ARDHI OFISINI
Mhe Silaa amesisitiza agizo alilolitoa hivi karibuni mjini Arusha, kuwataka wataalamu wa ardhi nchini kutumia siku mbili za Jumatatu na Ijumaa kukaa ofisini, na siku zinazosalia za Jumanne, Jumatano na Alhamis kwenda maeneo ya taaluma zao kufanya kazi kwa wananchi.
Amesema katika kutimiza agizo hilo, kila mtaalamu wa ardhi anatakiwa kuwa na kitabu cha kutunza kumbukumbu maarufuku kama Log Book, kitakachosainiwa na watendaji kata, mitaa na vijiji.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian, amesema hoja za Mhe Silaa zimejikita katika uelimishaji wa masuala mbalimbali yanayohusiana na haki za ardhi, hivyo kuifanya kliniki hiyo kuwa na manufaa zaidi ya utatuzi wa migogoro.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.