Na Mashaka Mgeta, KOROGWE
MKOA wa Tanga unaendelea kutekeleza mkakati wa uboreshaji elimu kupitia Mradi wa Shule Bora unaotekelezwa na Serikali kwa ufadhili wa Shirika la Misaada ya Uingereza (UK Aid).
Maafisa Elimu, Wadhibiti Ubora, Walimu Wakuu na Walimu wa kawaida wapatao 88 kutoka ngazi za Mkoa, Halmashauri na Kata mkoani humo, wanashiriki kikao kazi hicho cha siku mbili kinachofanyika wilayani Korogwe.
Katibu Tawala Mkoa (RAS) wa Tanga, Pili Mnyema, anasema ujuzi, ubunifu na mbinu mpya za ufundishaji na ujifunzaji ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufaulu hususani kwa masomo lengwa ya Kingereza na Hisabati.
Mnyema, aliyewakilishwa na Afisa Elimu - Taaluma Mkoa wa Tanga, Irine Makungu, amesema mradi wa Shule Bora umeleta mabadiliko kwenye sekta hiyo, akitoa mfano wa kupanda kwa ufaulu katika mitihani ya darasa la saba kutoka asilimia 70 ya mwaka 2023/2024 hadi asilimia 74 ya 2024/2025.
Mnyema, amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kutengeneza Mpango Kazi utakaokuwa chachu ya kuongeza uzito alama kwenye matokeo ya mitihani, na hivyo kuzidi kuinunua kiwango cha ufaulu.
Kwenye kikao hicho, washiriki hao walishirikishana uzoefu wa mafanikio kwa shule zilizo na ufaulu wa juu wa masomo hayo na zenye ufaulu wa chini kwa mitihani ya mwaka jana.
“Tunapotoka kwenye kikao kazi hiki, tuhakikishe tunakuwa wabobezi wa kuleta mabadiliko katika ufundishaji na ujifunzaji, tuongeze uzito wa alama ili wanafunzi wapate madaraja A na B,’’ anasema.
Kiongozi Mratibu wa Mradi wa Shule Bora, Petronia Kimizye, anasema washiriki wa kikao hicho wamegawanywa kwenye makundi mbalimbali ili kuunda mkakati ulio madhubuti utaowezesha kuinua ufaulu wa Kingereza na Hisabati.
Alisema awali, palikuwa na mikakati tofauti inayopaswa kuunganishwa na kuwa mmoja utakaotumika kwenye shule zote mkoani Tanga
Afisa Elimu wa Jiji la Tanga, Mwalimu Shomari Bane, amesema usahihishaji wa mitihani haupaswi kufanywa na wanafunzi wa madarasa ya juu kwa kazi za darasani za wanafunzi wa madarasa ya chini.
Alikuwa akichangia hoja kuhusu, kama ni sahihi kwa walimu kuwapa wanafunzi wa madarasa ya juu, jukumu la kusahihisha kazi za darasani za wanafunzi wa madarasa ya chini.
Naye Mratibu wa Shule Bora mkoani Tanga, Mwalimu Joseph Shayo, amesema kupitia kikao kazi hicho, wigo wa ufanisi katika sekta ya elimu, ikiwemo ufaulu hasa wa masomo ya Kiingereza na Hisabati, utafunguka na kupandisha ufaulu mkoani humo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.