Na Emma Kigombe, TANGA
WAZIRI wa Maji, Mhe Jumaa Aweso, Januari 17, mwaka huu, amekabidhi vifaa vya umaliziaji wa Mradi wa Maji wa Mkinga–Horohoro unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA).
Mradi huo unaogharimu Shilingi bilioni 35.7, unalenga kuongeza upatikanaji maji safi na salama kwa asilimia 40 katika Wilaya ya Mkinga.
Utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka 2022, na jiwe la msingi liliwekwa Februari 2025 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe Aweso, amewaelekeza watendaji kusimamia mradi huo kwa karibu,, ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa ni mabomba yenye thamani ya Shilingi bilioni 7.77, yatakayolazwa kwa umbali wa kilomita 91 na kusambaza maji kwa mtandao wa kilomita 104.
Akielezea changamoto ya muda mrefu ya maji katika Wilaya ya Mkinga, Mhe Aweso amesema, jiografia ya eneo hilo imekuwa kikwazo kikubwa, kwani licha ya kuchimba maji chini ya ardhi, hayakuwa salama kwa matumizi ya binadamu kutokana na ukaribu wa wilaya hiyo na bahari ya Hindi.
Amepongeza hatua ya kuwatumia wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mikubwa ya maji, akisema ni mapinduzi makubwa katika sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, amewataka watendaji kuhakikisha mabomba yaliyokabidhiwa yanalazwa na kufukiwa kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, amesema mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo na utakapokamilika utaondoa kwa kiasi kikubwa adha ya ukosefu wa maji safi na salama.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.