Na Mwandishi Wetu, OMM TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amewataka wakazi mkoani humo, kudumisha amani na utulivu, hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mhe Balozi Dkt Batilda, ametoa rai hiyo kwa nyakati tofauti, alipozungumza kwenye mikutano ya mabaraza maalumu ya madiwani ya kupitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) katika halmashauri za wilaya za Muheza, Mkinga na Jiji la Tanga.
Hata hivyo, amepongeza umoja na mshikamano wa wakazi hao bila kujali tofauti za itikadi, hivyo kuwasihi waiendeleze hali hiyo ili kuwa mfano mzuri wa maeneo mengine.
"Utulivu ambao tunauona mkoa wa Tanga ni mfano mzuri ambao Watanzania tunapaswa kuwa, vyama vyote vya siasa yaani chama tawala na vyama rafiki, sisi hatuiti vya upinzani, ni rafiki kwa sababu tunajua umoja wa Watanzania hautenganishwi kwa itikadi," amesema.
Ameongeza, "vyama vinashirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo bila kuzusha taharuki, hili tunapaswa kulidumisha."
Pia, Mhe Balozi Dkt Batilda, amewataka Watanzania kuwapuuza watu wachache wanaofanya uchochezi, kwani lengo lao ni kuona amani ya nchi inatoweka kwa maslahi yao binafsi.
Mkuu wa Mkoa huyo, ametoa wito kwa watumishi wa umma kwenda kwa wananchi vijijini kutatua kero zao.
"Rais wetu, Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan anatuhimiza kwenda kwa wananchi kutatua kero zao, anatuhimiza kuzingatia utu katika kuhudumia wananchi, ndio maana CCM imekuja na kauli mbiu ya 'Kazi na utu, tunasonga mbele,' amesema.
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, Tanzania inaelekea katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu, hivyo watanzania wanatakiwa kudumisha umoja na mshikamano kulinda amani ya nchi ni kutowapa mwanya wenye nia mbaya ya kuleta machafuko.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.