Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
DHANA ya ‘adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe’ inaondoka, shangwe ya upendo, umoja na ushirikiano miongoni mwao inashamiri, inakuwa sehemu ya mafanikio ya mchango wao kwenye jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, analiona hilo, na akizungumza kwenye Kongamano la Mabinti na Wanawake mkoani humo, anasema hivi sasa kuna viashiria vya wanawake kupendana, kusaidiana na kusemeana mambo mazuri.
Kwenye kongamano hilo lililoandaliwa na taasisi ya Mwanamke na Uongozi inayoongozwa na Shamira Mshangama, Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, hali hiyo ni tofauti na awali ilipojengeka dhana, hatimaye kuwafanya wanawake kuhusishwa na kusemana vibaya, husda na chuki miongoni mwao.
Anasema, kuondoka kwa dhana hiyo kumechochewa (kwa sehemu kubwa) na namna Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, anavyodhihirisha umahiri wake katika uongozi na kutoa fursa sawa kwa makundi ya kijamii, yanayowafanya (wanawake) kuonesha uwezo wao.
Amesema, ufanisi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020 – 2025 unaofanywa na Mhe Rais Dkt Samia, umewezesha kufikisha huduma za kijamii kwenye maeneo yote nchini, akitoa mfano wa Tanga kupokea takribani Shilingi trilioni 3.2 za miradi ya maendeleo kwa kipindi cha uongozi wake.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa CCM wa Mkoa wa Tanga, Al Shymaa Kwegyir, amewataka wanawake na wasichana kuwa miongoni mwa wabeba maono na mafanikio ya utendaji kazi bora wa Mhe Rais Dkt Samia, na kuyaeneza kwenye jamii katika maeneo yao.
Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Mhe Rehema Mhina amesema kongamano hilo lenye kauli mbiu inayosema, ‘ninasimama na Mama’, linapaswa kuwa chachu ya kueneza mafanikio wanayoyapata wanawake na wasichana katika huduma bora za afya, fursa za elimu na mikopo hususani inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.