Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, ameitahadharisha jamii kudhibiti umwagikaji mafuta baharini, ili kuepukana na madhara dhidi ya viumbe hai na mazingira.
Mhe Balozi Dkt Batilda, ametoa rai hiyo leo Machi 12, 2025, wakati akifungua warsha ya mazoei juu ya mpango wa taifa wa kujiandaa na kupambana na umwagikaji wa mafuta kwenye bahari na maziwa inayofanyika mkoani humo.
Amesema, taarifa za kitaalamu hususani kutoka Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) zinaeleza kuwa kiasi cha kuanzia galoni sita za mafuta zenye ujazo wa lita tano kila moja, zinapomwagika baharini ama kwenye maziwa, inahesabika kuwa ni umwagikaji wenye madhara makubwa kwa viumbe hai na mazingira.
Mhe Balozi Dkt Batilda anasema, miongoni mwa madhara yanayotokana na umwagikaji mafuta huo ni uharibifu wa ekolojia ya bahari, kuua viumbe hai wa majini wakiwemo Samaki na kuharibu asili ya maumbile ya bahari na maziwa.
Amesema, ipo haja kwa wadau wote wa hifadhi ya bahari na maziwa dhidi ya umwagikaji wa mafuta, kupata mbinu na stadi kupitia mafunzo yanayotolewa, ili kukuza na kuendeleza hifadhi, hivyo kulinda mazao ya baharini wakiwemo samaki na mimea kama mwani, unaochangia kuwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa buluu mkoani humo.
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, ataitisha kikao cha wadau wa sekta hiyo ili kujadili masuala mbalimbali, kwa kujumuisha pia namna bora ya utunzaji na uratibu wa vifaa vilivyotolewa na Marine Park kwa ajili ya masuala yanayohusiana na udhibiti wa umwagikaji mafuta baharini.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usalama, Ulinzi na Utunzaji Mazingira (DMSE) wa TASAC, Leticia Mutaki, amesema wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wamealikwa kushiriki mafunzo hayo yatakayohusisha zoezi la kukabiliana na umwagikaji wa mafuta kwenye fukwe za bahari ya Hindi.
Abubakar Ali Almas kutoka Shirika la Bandari Zanzibar, amesema mafunzo hayo ni moja yah atua muhimu zinazochangia uimarishaji wa mazingira ya bahari, na kuvifanya viumbe hai na mazao mengine ya baharini kuwa endelevu.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.