Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
MSEMO wa “umoja na nguvu”, umetafsiriwa kwa vitendo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, kuwakutanisha viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumshukuru Mungu kwa kufanikisha ziara ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan mkoani humo.
Mhe Rais Dkt Samia alifanya ziara kati ya Februari 23 na Machi Mosi, 2025, ambapo alikagua, kuweka jiwe la msingi, kufungua miradi na kuzungumza na wananchi kwenye wilaya zote nane za Tanga.
Iftar hiyo iliyohudhuriwa na Mshauri wa Rais (Siasa na Mambo ya Jamii), Haji Omar Heri ilifanyika jana jioni nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa.
Ni mjumuiko unaowaleta Serikali na Chama pamoja, kupitia tukio la ‘ki-sadaka’ la kushiriki Iftar, huku wakitathmini na kumshukuru Mwenyezi Mungu kuisimamia ziara hiyo ya siku sita.
Mhe Balozi Dkt Batilda akasema, si rahisi akajitokeza mtu mmoja kujinasibu kuwa amefanikisha ziara hiyo pasipo ushiriki wa wengine.
“Kuanzia viongozi wa mkoa hadi mwananchi wa kawaida, wana Tanga wote tuna mkono wetu katika ufanisi na mafanikio yaliyotufanya tuuone upendo mkubwa wa Mh Rais Dkt Samia kuja hapa kwetu,” amesema.
Mshauri wa Rais (Siasa na Mambo ya Jamii), Heri, alipongeza ushirikiano wa viongozi wa Serikali, Chama na asasi za kiraia mkoani humo, na kusihi kuendelezwa.
Mwenyekiti wa CCM (M), Abdallah akasema umati wa watu waliojitokeza kwenye ziara hiyo, unaashiria wakazi wa Tanga wanavyomkubali Mhe Rais Dkt Samia.
Amesema kukubalika kwa Mhe Rais Dk Samia, kunatokana na utendaji kazi na utekelezaji wa ahadi zake, akitoa mfano wa kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 763 za mkoani Tanga, ikiwa ni kabla muda uliokusudiwa wa Desemba 2025.
Mfano mwingine ni kupatikana maji kwa asilimia 96 mijini na asilimia 75 vijijini, huku kazi ya usambazi wa rasilimali hiyo muhimu kwa maisha na mazingira ikiendelea.
Kwa hali hiyo, Abdallah ametoa rai kwa viongozi na watendaji serikalini mkoani Tanga, kuwekeza zaidi katika kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Pia, Abdallah amesema ushirikiano uliooneshwa kabla na wakati wa ziara ya Mhe Rais Dkt Samia, uendelezwe katika utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa, ikiwemo kuirejesha Tanga kuwa jiji la viwanda.
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe Abdurahaman Shiloow, amesema ipo haja ya kuendeleza imani ya wananchi wengi waliojitokeza kumlaki kwenye ziara ya Mhe Rais Dkt Samia, ili kwa umoja huo, wampigie kura kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.